Thursday 24 August 2017

Ndugu wasusia mwili wa jamaa yao aliyefariki kwa utata

Ndugu wa marehemu Shinje Charles mwenye umri wa miaka 25, mkazi wa mtaa wa Uwanja, kata ya Nyankumbu mjini Geita, wamesusia kuchukua mwili wa ndugu yao, kutokana na utata wa kifo chake mpaka uchunguzi utakapokamilika.                       

Inadaiwa marehemu Charles amefariki dunia kufuatia kipigo alichopokea kutoka kwa walinzi wa mgodi wa Geita Gold Mine uliopo mkoani Geita.

Wakisimulia kifo cha kijana huyo vijana wawili Philipo Enock na Shija Mashema wamesema mnamo Agosti 21, mwaka huu,waliingia katika eneo la mgodi wa GGM kwa lengo la kuiba mabaki ya mawe ya dhahabu (magwangala).

Vijana hao wamesema wakati wakiwa njiani, walinzi hao waliwaona na kuanza kuwakimbiza, ndipo marehemu alipokamatwa.                       

Mashuhuda hao wameongeza kuwa hadi mwenzao Charles anakamatwa, bado alikuwa hai na alibebwa kwenye gari la walinzi hao na kuondoka naye.

Vijana hao wamesema walikimbilia kwenye mashimo madogo na kujificha kwa muda wa siku mbili, na baadae kuarifiwa kwa simu kuwa mwenzao amefariki dunia na mwili wake umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya mkoa Geita.

Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt. Joseph Kisalo,  amethibitisha kupokea mwili wa marehemu huyo, huku afisa uhusiano wa jamii na GGM  Manase Ndoroma, akikiri kutokea kwa tukio hilo japo amekanusha madai ya kupigwa kwa kijana huyo.

 Kwa mujibu wa taarifa ya mwandishi wa Azam TV Ester Sumira aliyopo mkoani Geita, afisa uhusiano huyo amedai kuwa kijana huyo alianguka kwenye kuta za shimo la mgodi.    

Monday 21 August 2017

JPM amteua brigedia kuwa naibu mkurugenzi TAKUKURU

Rais John Magufuli leo Agosti 21, amemteua brigedia jenerali John Julius Mbungo, kuwa naibu mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu, Gerson Msigwa, uteuzi wa brigedia Mbungo, umeanza leo.

Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa (TAKUKURU) ni ya umma, iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007.

Sheria hiyo ilitungwa baada ya kufutwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) sura ya 329, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Kuanzishwa kwa chombo hicho kulikuja baada ya Bunge la Tanzania, kupitisha muswada wa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2007 mnamo Aprili 6.

Muswada huo ulisainiwa na rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, na kuwa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mnamo Juni 11, 2007 na ilianza kufanya kazi Julai mwaka huo.

Sunday 6 August 2017

TCAA YAKANA KUITAMBUA NDEGE YA GWAJIMA

Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imekana kuwa na taarifa ya ndege iliyonunuliwa na Askofu wa Kanisa Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima nchini Marekani.

Juzi, Askofu Gwajima alithibitisha kununua ndege hiyo aina ya GulfStream N60983 yenye thamani ya Sh2.64 bilioni kwa ajili ya kuitumia kusambaza injili.

Ili kuonyesha msisitizo, Askofu Gwajima aliweka picha kwenye mitandao ya kijamii iliyomwonyesha mbele ya ndege hiyo.

Kiongozi huyo wa dini alisema ameijaribisha ndege hiyo kwa kusafiri viwanja tofauti nchini Marekani na kuridhika nayo.

Hata hivyo, akieleza utaratibu wa kuiingiza nchini, Ofisa Habari wa TCAA, Ali Changwila alisema mamlaka hiyo haina taarifa ya ununuzi wa ndege hiyo.

Alisema Mtanzania yeyote anayenunua ndege nje ya nchi kuiingiza nchini anatakiwa kwanza kuitaarifu mamlaka hiyo ili ifahamu na kuwa na taarifa nayo.
"Nimejiridhisha kwa wataalamu wetu, hakuna taarifa yoyote ya ununuzi wa hiyo hapa ofisini", alisema Changwila na kuongeza:

"Kwa kawaida mtu anapotaka kununua ndege na kuileta Tanzania, kwanza lazima aje TCAA atuambie ni ndege ya aina gani ili tujue kama wataalamu wetu wanaifahamu. Kama hawaifahamu inabidi awape mafunzo ili waweze kuikagua hiyo ndege ikiwa nje ya nchi".

Hata hivyo, alisema TCAA ina wataalamu waliobobea katika urubani na uhandisi wa ndege walio tayari kufanya ukaguzi wa ndege mbalimbali zinazoingizwa nchini.

Alisema hatua ya kwanza ni wataalamu hao kwenda ilikonunuliwa ndege husika na kuikagua kama inakidhi vigezo vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
"Je imekidhi vigezo vya ICAO? Inacho cheti cha kusajiliwa? Historia yake ikoje? Imekwisha muda wake? Imeshakatwazwa kusafiri? Maana kuna ndege zimeshapitisha muda wa kutumia halafu zinauzwa", alisema Changwila.

Ofisa huyo aliongeza kuwa baada ya wataalamu wao kujiridhisha, mwenye ndege atatakiwa kujaza fomu ya TCAA ili kufuata sheria za ndani na pia ataeleza ndege hiyo itaendeshwa na rubani gani na itatumika katika viwanja gani.

"Ni kama tu unataka leseni ya biashara, lazima ukidhi vigezo", alisisitiza Changwila.
"Wapo Watanzania walionunua ndege na wamefuata masharti hayo, kwa mfano Precision Air inamilikiwa na Watanzania, Coastal Aviation, hata marehemu Philemon Ndesamburo alikuwa akimiliki helkopta kwa kufuata masharti hayo.

Wednesday 2 August 2017

Urusi: Marekani imetangaza ''vita vya kibiashara'' kwetu

Waziri mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev amesema kuwa vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani dhidi ya taifa hilo ni sawa na kutangaza vita vya kibiashara.

Amesema kuwa mikakati iliotiwa saini na rais Trump inaonyesha udhaifu wa rais huyo wa Marekani ambaye alisema ameaibishwa na bunge la Congress.

Sheria hiyo inalenga kuiadhibu Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani wa 2016 pamoja na vitendo vyake dhidi ya Ukraine.

Katika kutia saini makubaliano hayo dhidi ya adui wa Marekani kupitia sheria ya vikwazo siku ya Jumatano, aliweka taarifa akisema kuwa mkakati huo sio wa sawa.

Sheria hiyo pia inaiwekea vikwazo Iran na Korea Kaskazini, Iran imesema kuwa vikwazo hivyo vipya vinakiuka makubaliano ya mpango wa nyuklia na kwamba itajibu kwa njia ilio ''sahihi na sawia'' kulingana na chombo cha habari cha Isna.

Korea Kaskazini kwa upande wake haijatoa matamshi yoyote kuhusiana na hatua hiyo ya Marekani.
Bwana Medvedev pia alionya kwamba hatua mpya zinazolenga kumuondoa rais Trump madarakani zitachukuliwa kwa kuwa sio mtu aliye na utaratibu.

Moscow ambayo imekana kuingilia uchaguzi wa Marekani tayari imelipiza kisasi wiki iliopita wakati bunge la Congress lilipopitisha muswada uliowatimua maafisa 755 kutoka katika ubalozi wa Marekani nchini Urusi mbali na kuzuiwa kutumia jengo moja la Marekani pamopja na ghala moja nchini Moscow.

Mataifa kadhaa ya Ulaya ikiwemo Ujerumani yanahofia vikwazo hivyo vipya na rais wa tume ya Ulaya Jean Claude Juncker ameonya kwamba athari yake itaathiri maslahi ya kawi ya Ulaya.

Marekani yakana kutaka kuing’oa Korea Kaskazini

Serikali ya Marekani kupitia waziri wa maswala ya kigeni Rex Tillerson, imesema haina dhamira ya kuing’oa madarakani utawala wa Korea Kaskazini, wakati huu ambao kumekuwa na hali ya wasiwasi juu ya mpango wa silaha za nyuklia wa Pyongyang.

 “Sisi siyo maadui” alisema Tillerson na kuongeza kuwa Marekani ilihitaji majadiliano kwa kiasi fulani.

Pamoja na kauli ya waziri huyo, seneta mmoja mwandamizi wa Chama cha Republican amesema rais Trump amelipa uzito suala la kuingia kwenye vita na taifa hilo la Korea Kaskazini, akiamini kuwa hilo ndilo chaguo sahihi.

Yenyewe Korea Kaskazini inadai kuwa jaribio lake la hivi karibuni la kombora la masafa marefu, linaweza kupiga pwani ya Magharibi ya Marekani na sehemu nyingine.

“Hatutafuti mabadiliko ya madaraka, hatutafuti anguko la utawala, sisi siyo maadui zenu, sisi siyo tishio kwenu, lakini mnawasilisha tishio lisilokubalika kwetu na tunapaswa kujibu,” alisema Tillerson akiiambia Korea Kaskazini.

Watoto walioungana kutengenishwa baada ya miezi sita

Daktari Bingwa Hospitali ya Taifa Muhimbili aliyebobea katika fani ya upasuaji wa watoto Afrika Mashariki, Zaituni Bokhari amesema baada ya kufanya vipimo, imegundulika kuna uwezekano wa kuwatenganisha watoto mapacha waliozaliwa wakiwa wameungana.

Dk Bokhari ameyasema hayo leo Jumatano alipokuwa akitoa majibu ya vipimo vilivyochukuliwa hospitalini hapo kwa takriban wiki nzima.

“Vipimo vya damu vimeonyesha kila mtoto ana mfumo wake na hawana maambukizi ya aina yoyote, ugumu unakuja kwenye ini na moyo ambapo wanategemeana ila uwezekano wa kutenganishwa upo,” amesema Dk Bokhari.

Majibu hayo yamekuja siku chache baada ya pacha hao kupimwa vipimo vya radiolojia ikiwemo CT Scan, MRI, X Ray kipimo cha moyo (ECO) pamoja na vipimo vyote vya damu.

Watoto hao waliozaliwa katika hospitali ya Misheni ya Berega iliyopo Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro, Julai 21 mwaka huu wamenaza kuchukuliwa vipimo mbalimbali vya awali.