Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imekana kuwa na taarifa ya ndege iliyonunuliwa na Askofu wa Kanisa Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima nchini Marekani.
Juzi, Askofu Gwajima alithibitisha kununua ndege hiyo aina ya GulfStream N60983 yenye thamani ya Sh2.64 bilioni kwa ajili ya kuitumia kusambaza injili.
Ili kuonyesha msisitizo, Askofu Gwajima aliweka picha kwenye mitandao ya kijamii iliyomwonyesha mbele ya ndege hiyo.
Kiongozi huyo wa dini alisema ameijaribisha ndege hiyo kwa kusafiri viwanja tofauti nchini Marekani na kuridhika nayo.
Hata hivyo, akieleza utaratibu wa kuiingiza nchini, Ofisa Habari wa TCAA, Ali Changwila alisema mamlaka hiyo haina taarifa ya ununuzi wa ndege hiyo.
Alisema Mtanzania yeyote anayenunua ndege nje ya nchi kuiingiza nchini anatakiwa kwanza kuitaarifu mamlaka hiyo ili ifahamu na kuwa na taarifa nayo.
"Nimejiridhisha kwa wataalamu wetu, hakuna taarifa yoyote ya ununuzi wa hiyo hapa ofisini", alisema Changwila na kuongeza:
"Kwa kawaida mtu anapotaka kununua ndege na kuileta Tanzania, kwanza lazima aje TCAA atuambie ni ndege ya aina gani ili tujue kama wataalamu wetu wanaifahamu. Kama hawaifahamu inabidi awape mafunzo ili waweze kuikagua hiyo ndege ikiwa nje ya nchi".
Hata hivyo, alisema TCAA ina wataalamu waliobobea katika urubani na uhandisi wa ndege walio tayari kufanya ukaguzi wa ndege mbalimbali zinazoingizwa nchini.
Alisema hatua ya kwanza ni wataalamu hao kwenda ilikonunuliwa ndege husika na kuikagua kama inakidhi vigezo vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
"Je imekidhi vigezo vya ICAO? Inacho cheti cha kusajiliwa? Historia yake ikoje? Imekwisha muda wake? Imeshakatwazwa kusafiri? Maana kuna ndege zimeshapitisha muda wa kutumia halafu zinauzwa", alisema Changwila.
Ofisa huyo aliongeza kuwa baada ya wataalamu wao kujiridhisha, mwenye ndege atatakiwa kujaza fomu ya TCAA ili kufuata sheria za ndani na pia ataeleza ndege hiyo itaendeshwa na rubani gani na itatumika katika viwanja gani.
"Ni kama tu unataka leseni ya biashara, lazima ukidhi vigezo", alisisitiza Changwila.
"Wapo Watanzania walionunua ndege na wamefuata masharti hayo, kwa mfano Precision Air inamilikiwa na Watanzania, Coastal Aviation, hata marehemu Philemon Ndesamburo alikuwa akimiliki helkopta kwa kufuata masharti hayo.
0 comments:
Post a Comment