Thursday 24 August 2017

Ndugu wasusia mwili wa jamaa yao aliyefariki kwa utata

Ndugu wa marehemu Shinje Charles mwenye umri wa miaka 25, mkazi wa mtaa wa Uwanja, kata ya Nyankumbu mjini Geita, wamesusia kuchukua mwili wa ndugu yao, kutokana na utata wa kifo chake mpaka uchunguzi utakapokamilika.                       

Inadaiwa marehemu Charles amefariki dunia kufuatia kipigo alichopokea kutoka kwa walinzi wa mgodi wa Geita Gold Mine uliopo mkoani Geita.

Wakisimulia kifo cha kijana huyo vijana wawili Philipo Enock na Shija Mashema wamesema mnamo Agosti 21, mwaka huu,waliingia katika eneo la mgodi wa GGM kwa lengo la kuiba mabaki ya mawe ya dhahabu (magwangala).

Vijana hao wamesema wakati wakiwa njiani, walinzi hao waliwaona na kuanza kuwakimbiza, ndipo marehemu alipokamatwa.                       

Mashuhuda hao wameongeza kuwa hadi mwenzao Charles anakamatwa, bado alikuwa hai na alibebwa kwenye gari la walinzi hao na kuondoka naye.

Vijana hao wamesema walikimbilia kwenye mashimo madogo na kujificha kwa muda wa siku mbili, na baadae kuarifiwa kwa simu kuwa mwenzao amefariki dunia na mwili wake umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya mkoa Geita.

Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt. Joseph Kisalo,  amethibitisha kupokea mwili wa marehemu huyo, huku afisa uhusiano wa jamii na GGM  Manase Ndoroma, akikiri kutokea kwa tukio hilo japo amekanusha madai ya kupigwa kwa kijana huyo.

 Kwa mujibu wa taarifa ya mwandishi wa Azam TV Ester Sumira aliyopo mkoani Geita, afisa uhusiano huyo amedai kuwa kijana huyo alianguka kwenye kuta za shimo la mgodi.    

0 comments:

Post a Comment