Wednesday 26 July 2017

Shilingi 180,000 za mjamzito zamtokea puani mganga mkuu

Waziri wa afya, Ummy Mwalimu amemsimamisha kazi mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Mlandizi, Stanley Mpola  kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo alipotembelea kituo hicho cha afya kabla ya kukabidhi magari matatu ya kubebea wagonjwa, mawili yakiwa yametolewa na mbunge wa Kibaha Vijijini, Amoud Jumaa na moja likiwa ni ahadi ya Rais John Magufuli.

Akiwa katika kituo hicho waziri huyo alipewa malalamiko kutoka kwa mama mmoja aitwaye Salma Halfan aliyedai  kufanyiwa upasuaji katika kituo hicho na kutozwa  gharama ya vifaa vya upasuaji kiasi cha shilingi 180, 000.

Hata hivyo mganga huyo alimweleza waziri kuwa fedha hizo hazikutolewa katika kituo hicho bali mgonjwa huyo alipewa orodha ya vifaa akaenda kununua mwenyewe duka la dawa.

Hata hivyo Waziri Ummy alisema gharama za vifaa hivyo ni kubwa ukilinganisha na hali halisi ya upasuaji huku akiwatupia lawama watumishi wa afya kuwa hata maduka ya dawa wanayoelekeza wagonjwa wamiliki wake ni wao wenyewe.

" Tunajigamba huduma kwa wanawake wanaokwenda kujifungua ni bure, halafu nyie mnawachaji wanawake wajawazito, hii orodha mliyompa ni kweli vifaa vyote hivi hakuna, na hizi gloves 17 alizonunua ni za nini, ni kweli zinatumika zote,  hamna hata huruma, wanawake wajawazito mmewafanya mtaji, kuna haja gani ya kuja katika kituo cha afya wakati gharama zinazidi zile za hosptali binafsi," amesema Waziri Ummy.

Waziri huyo aliagiza apate orodha ya wauguzi wote waliokuwa zamu siku hiyo na waliomuhudumia mgonjwa huyo ili waweze kuchukuliwa hatua .

"Orodha yote ya waliohusika kumuhudumia mgonjwa huyu niipate kesho, nitarudi tena kuongea na watumishi, na huyu mama naagiza ahamishiwe hospitali ya rufaa Tumbi kwa usalama wake, mnaweza mkafanya lolote amekuwa jasiri kunieleza kero yake, na ole wake mtumishi wa afya atakayemfanyia kitendo kibaya mjamzito naahidi kula naye sahani moja," amesema Ummy.

"Alisema ilani ya uchaguzi ni pamoja na matibabu bure kwa wajawazito, watoto chini ya umri wa miaka mitano na wazeee wasiojiweza hivyo  serikali kwa kuhakikisha inatekeleza ilani yake haitamvumilia mtumishi yeyote wa afya atayeshindwa kutoa huduma bora za afya kwa wananchi."

0 comments:

Post a Comment