Sunday, 6 August 2017

TCAA YAKANA KUITAMBUA NDEGE YA GWAJIMA

Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imekana kuwa na taarifa ya ndege iliyonunuliwa na Askofu wa Kanisa Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima nchini Marekani.

Juzi, Askofu Gwajima alithibitisha kununua ndege hiyo aina ya GulfStream N60983 yenye thamani ya Sh2.64 bilioni kwa ajili ya kuitumia kusambaza injili.

Ili kuonyesha msisitizo, Askofu Gwajima aliweka picha kwenye mitandao ya kijamii iliyomwonyesha mbele ya ndege hiyo.

Kiongozi huyo wa dini alisema ameijaribisha ndege hiyo kwa kusafiri viwanja tofauti nchini Marekani na kuridhika nayo.

Hata hivyo, akieleza utaratibu wa kuiingiza nchini, Ofisa Habari wa TCAA, Ali Changwila alisema mamlaka hiyo haina taarifa ya ununuzi wa ndege hiyo.

Alisema Mtanzania yeyote anayenunua ndege nje ya nchi kuiingiza nchini anatakiwa kwanza kuitaarifu mamlaka hiyo ili ifahamu na kuwa na taarifa nayo.
"Nimejiridhisha kwa wataalamu wetu, hakuna taarifa yoyote ya ununuzi wa hiyo hapa ofisini", alisema Changwila na kuongeza:

"Kwa kawaida mtu anapotaka kununua ndege na kuileta Tanzania, kwanza lazima aje TCAA atuambie ni ndege ya aina gani ili tujue kama wataalamu wetu wanaifahamu. Kama hawaifahamu inabidi awape mafunzo ili waweze kuikagua hiyo ndege ikiwa nje ya nchi".

Hata hivyo, alisema TCAA ina wataalamu waliobobea katika urubani na uhandisi wa ndege walio tayari kufanya ukaguzi wa ndege mbalimbali zinazoingizwa nchini.

Alisema hatua ya kwanza ni wataalamu hao kwenda ilikonunuliwa ndege husika na kuikagua kama inakidhi vigezo vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
"Je imekidhi vigezo vya ICAO? Inacho cheti cha kusajiliwa? Historia yake ikoje? Imekwisha muda wake? Imeshakatwazwa kusafiri? Maana kuna ndege zimeshapitisha muda wa kutumia halafu zinauzwa", alisema Changwila.

Ofisa huyo aliongeza kuwa baada ya wataalamu wao kujiridhisha, mwenye ndege atatakiwa kujaza fomu ya TCAA ili kufuata sheria za ndani na pia ataeleza ndege hiyo itaendeshwa na rubani gani na itatumika katika viwanja gani.

"Ni kama tu unataka leseni ya biashara, lazima ukidhi vigezo", alisisitiza Changwila.
"Wapo Watanzania walionunua ndege na wamefuata masharti hayo, kwa mfano Precision Air inamilikiwa na Watanzania, Coastal Aviation, hata marehemu Philemon Ndesamburo alikuwa akimiliki helkopta kwa kufuata masharti hayo.

Wednesday, 2 August 2017

Urusi: Marekani imetangaza ''vita vya kibiashara'' kwetu

Waziri mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev amesema kuwa vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani dhidi ya taifa hilo ni sawa na kutangaza vita vya kibiashara.

Amesema kuwa mikakati iliotiwa saini na rais Trump inaonyesha udhaifu wa rais huyo wa Marekani ambaye alisema ameaibishwa na bunge la Congress.

Sheria hiyo inalenga kuiadhibu Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani wa 2016 pamoja na vitendo vyake dhidi ya Ukraine.

Katika kutia saini makubaliano hayo dhidi ya adui wa Marekani kupitia sheria ya vikwazo siku ya Jumatano, aliweka taarifa akisema kuwa mkakati huo sio wa sawa.

Sheria hiyo pia inaiwekea vikwazo Iran na Korea Kaskazini, Iran imesema kuwa vikwazo hivyo vipya vinakiuka makubaliano ya mpango wa nyuklia na kwamba itajibu kwa njia ilio ''sahihi na sawia'' kulingana na chombo cha habari cha Isna.

Korea Kaskazini kwa upande wake haijatoa matamshi yoyote kuhusiana na hatua hiyo ya Marekani.
Bwana Medvedev pia alionya kwamba hatua mpya zinazolenga kumuondoa rais Trump madarakani zitachukuliwa kwa kuwa sio mtu aliye na utaratibu.

Moscow ambayo imekana kuingilia uchaguzi wa Marekani tayari imelipiza kisasi wiki iliopita wakati bunge la Congress lilipopitisha muswada uliowatimua maafisa 755 kutoka katika ubalozi wa Marekani nchini Urusi mbali na kuzuiwa kutumia jengo moja la Marekani pamopja na ghala moja nchini Moscow.

Mataifa kadhaa ya Ulaya ikiwemo Ujerumani yanahofia vikwazo hivyo vipya na rais wa tume ya Ulaya Jean Claude Juncker ameonya kwamba athari yake itaathiri maslahi ya kawi ya Ulaya.

Marekani yakana kutaka kuing’oa Korea Kaskazini

Serikali ya Marekani kupitia waziri wa maswala ya kigeni Rex Tillerson, imesema haina dhamira ya kuing’oa madarakani utawala wa Korea Kaskazini, wakati huu ambao kumekuwa na hali ya wasiwasi juu ya mpango wa silaha za nyuklia wa Pyongyang.

 “Sisi siyo maadui” alisema Tillerson na kuongeza kuwa Marekani ilihitaji majadiliano kwa kiasi fulani.

Pamoja na kauli ya waziri huyo, seneta mmoja mwandamizi wa Chama cha Republican amesema rais Trump amelipa uzito suala la kuingia kwenye vita na taifa hilo la Korea Kaskazini, akiamini kuwa hilo ndilo chaguo sahihi.

Yenyewe Korea Kaskazini inadai kuwa jaribio lake la hivi karibuni la kombora la masafa marefu, linaweza kupiga pwani ya Magharibi ya Marekani na sehemu nyingine.

“Hatutafuti mabadiliko ya madaraka, hatutafuti anguko la utawala, sisi siyo maadui zenu, sisi siyo tishio kwenu, lakini mnawasilisha tishio lisilokubalika kwetu na tunapaswa kujibu,” alisema Tillerson akiiambia Korea Kaskazini.

Watoto walioungana kutengenishwa baada ya miezi sita

Daktari Bingwa Hospitali ya Taifa Muhimbili aliyebobea katika fani ya upasuaji wa watoto Afrika Mashariki, Zaituni Bokhari amesema baada ya kufanya vipimo, imegundulika kuna uwezekano wa kuwatenganisha watoto mapacha waliozaliwa wakiwa wameungana.

Dk Bokhari ameyasema hayo leo Jumatano alipokuwa akitoa majibu ya vipimo vilivyochukuliwa hospitalini hapo kwa takriban wiki nzima.

“Vipimo vya damu vimeonyesha kila mtoto ana mfumo wake na hawana maambukizi ya aina yoyote, ugumu unakuja kwenye ini na moyo ambapo wanategemeana ila uwezekano wa kutenganishwa upo,” amesema Dk Bokhari.

Majibu hayo yamekuja siku chache baada ya pacha hao kupimwa vipimo vya radiolojia ikiwemo CT Scan, MRI, X Ray kipimo cha moyo (ECO) pamoja na vipimo vyote vya damu.

Watoto hao waliozaliwa katika hospitali ya Misheni ya Berega iliyopo Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro, Julai 21 mwaka huu wamenaza kuchukuliwa vipimo mbalimbali vya awali.

Monday, 31 July 2017

Aliyeanzisha kampeni ya 'Magufuli Baki' akimbilia TCRA

Mmalaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeombwa kufuatilia kwa makini  mawasiliano ya simu za mkononi ili kubaini watu wanaotumia mitandao hiyo  kinyume na sheria.

Ombi hilo limetolewa na mwanaharakati Lawrence Mabawa  jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari vitisho anavyopata kupitia simu ya mkoni baada ya kutambulisha kampeni yake ya ‘BAKI MAGUFULI’.

Kwa mujibu wa Mabawa, baadhi ya wananchi wameelewa vibaya kampeni hiyo na kufikia hatua ya kutoa maneno ya matusi na kejeli kwake.

Akifafanua lengo la kampeni yake, Mabawa amesema alimaanisha  kuwa Rais abaki na msimamo wake ambao kwa kiasi kikubwa unapeleka taifa la Tanzania mbele kimaendeleo, na si kama ambavyo watu hao wameichukulia.

Thursday, 27 July 2017

Wanawake watano wafariki kwa kuchomwa moto Tabora

Watu watano wamefariki dunia kwa kuchomwa moto na watu wanaosaidikiwa kuwa ni sungusungu katika kata ya Uchama wilayani Nzega mkoani Tabora.

 

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, amezitaka Kamati za Ulinzi na usalama ngazi ya mkoa na ile ya Wilaya ya Nzega kusitisha shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na sungusungu katika kijiji hicho.

Mwanri amesema kuwa amechukua hatua hiyo baada ya sungusungu hao kutekeleza mauaji hayo ya watu watano ambao wote ni wanawake wakituhumiwa kuwa ni washirikina.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa amesema kuwa katika kuendelea kuchunguza tukio hilo jeshi hilo linawashikilia baadhi ya viongozi wa kijiji hicho ili kuweza kubaini waliotekeleza tukio hilo.

 

JPM 'aipa tano' TCU kwa kufungia vyuo

Rais John Magufuli ameipongeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuzuia udahili wa wanafunzi wote wa mwaka kwanza katika vyuo vikuu 19 na kuzuia udahili wa wanafunzi wa kozi 75 katika vyuo vikuu 22 kutokana na dosari zilizobainika wakati wa ukaguzi wa ubora vyuo hivyo uliofanyika Oktoba 2016.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo alipowasili jijini Dar es Salaam leo akitokea mkoani Dodoma ambapo akiwa katika eneo la Tegeta wilaya ya Kinondoni amezungumza na wananchi wa eneo hilo.

“Ndugu zangu nchi hii ilishakuwa kila kitu hewa hewa, tumegundua wafanyakazi hewa zaidi ya 19,500, kulikuwa na mikopo hewa ya wanafunzi, na naipongeza TCU kwa kufungia baadhi ya vyuo kudahili wanafunzi, nafanya yote haya kwa ajili yenu, nataka tuwe na nchi nzuri,” amebainisha rais Magufuli.

 Rais Magufuli ameahidi kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na kero na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.“Mimi nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote na kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Watanzania wote hasa wanyonge ambao siku zote walikuwa wakionewa,” amesema rais Magufuli

Baadhi ya juhudi alizozitaja kufanyika tangu aingie madarakani ni pamoja na kuondoa ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka shilingi bilioni 371 hadi kufikia shilingi bilioni 483, kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi na kulinda mali za umma hasa madini.

“Kwenye madini tumeibiwa sana, nchi yetu ni kati ya nchi zinazoongoza kwa kuibiwa, tumeibiwa kwa miaka 18, sasa imetosha,” amesisitiza rais Magufuli.

Wednesday, 26 July 2017

Serikali yatangaza ajira 3,152 sekta ya afya

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo imetangaza ajira 3,152 kwa ajili ya wahitimu wa kada mbalimbali za afya nchini.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na wizara hiyo, ajira hizo ambazo zinatolewa kwa kibali cha wizara ya utumishi na utawala bora, ni kwa ajili ya watumishi kutoka kada 33 za afya.

Baadhi ya kada zilizotangazwa ni pamoja na madaktari, wataalam wa maabara, wauguzi/wauguzi wasaidizi, matabibu wasaidizi, wataalam wa meno, wataalam wa afya ya mazingira, wataalam wa mionzi, wataalam wa takwimu za afya, makatibu muktasi katika sekta ya afya, wataalam wa usafi, washauri wa afya, wafamasia n.k

Ajira hizo zinawahusu wahitimu wote wenye sifa stahiki za kitaaluma na hazitawahusu wahitimu wenye umri zaidi ya miaka 45, wahitimu ambao tayari ni waajiriwa wa serikali au wa mashirika wanaolipwa na serikali, pia hazitawahusu watu wote ambao wamewahi kufanya kazi serikalini na kuacha.

Ujio wa ajira hizi, ni tulizo la nafsi kwa wahitimu ambao wamekuwa wakisubiri ajira serikalini kwa takriban miaka miwili tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, ambayo mwaka jana ilisitisha ajira kwa ajili ya kupisha zoezi uhakiki wa watumishi hewa.

Pia ajira hizo ni kuanza kwa utekelezaji wa mipango ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 ambapo mara kadhaa imekuwa ikiahidi kutoa ajira zaidi ya 50,000.

Waombaji wote wametakiwa kutuma maombi yao kabla ya Agosti 11 mwaka.

Shilingi 180,000 za mjamzito zamtokea puani mganga mkuu

Waziri wa afya, Ummy Mwalimu amemsimamisha kazi mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Mlandizi, Stanley Mpola  kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo alipotembelea kituo hicho cha afya kabla ya kukabidhi magari matatu ya kubebea wagonjwa, mawili yakiwa yametolewa na mbunge wa Kibaha Vijijini, Amoud Jumaa na moja likiwa ni ahadi ya Rais John Magufuli.

Akiwa katika kituo hicho waziri huyo alipewa malalamiko kutoka kwa mama mmoja aitwaye Salma Halfan aliyedai  kufanyiwa upasuaji katika kituo hicho na kutozwa  gharama ya vifaa vya upasuaji kiasi cha shilingi 180, 000.

Hata hivyo mganga huyo alimweleza waziri kuwa fedha hizo hazikutolewa katika kituo hicho bali mgonjwa huyo alipewa orodha ya vifaa akaenda kununua mwenyewe duka la dawa.

Hata hivyo Waziri Ummy alisema gharama za vifaa hivyo ni kubwa ukilinganisha na hali halisi ya upasuaji huku akiwatupia lawama watumishi wa afya kuwa hata maduka ya dawa wanayoelekeza wagonjwa wamiliki wake ni wao wenyewe.

" Tunajigamba huduma kwa wanawake wanaokwenda kujifungua ni bure, halafu nyie mnawachaji wanawake wajawazito, hii orodha mliyompa ni kweli vifaa vyote hivi hakuna, na hizi gloves 17 alizonunua ni za nini, ni kweli zinatumika zote,  hamna hata huruma, wanawake wajawazito mmewafanya mtaji, kuna haja gani ya kuja katika kituo cha afya wakati gharama zinazidi zile za hosptali binafsi," amesema Waziri Ummy.

Waziri huyo aliagiza apate orodha ya wauguzi wote waliokuwa zamu siku hiyo na waliomuhudumia mgonjwa huyo ili waweze kuchukuliwa hatua .

"Orodha yote ya waliohusika kumuhudumia mgonjwa huyu niipate kesho, nitarudi tena kuongea na watumishi, na huyu mama naagiza ahamishiwe hospitali ya rufaa Tumbi kwa usalama wake, mnaweza mkafanya lolote amekuwa jasiri kunieleza kero yake, na ole wake mtumishi wa afya atakayemfanyia kitendo kibaya mjamzito naahidi kula naye sahani moja," amesema Ummy.

"Alisema ilani ya uchaguzi ni pamoja na matibabu bure kwa wajawazito, watoto chini ya umri wa miaka mitano na wazeee wasiojiweza hivyo  serikali kwa kuhakikisha inatekeleza ilani yake haitamvumilia mtumishi yeyote wa afya atayeshindwa kutoa huduma bora za afya kwa wananchi."

Thursday, 13 July 2017

Ukosefu wa bangi wasababisha dharura kutangwazwa Nevada, Marekani

Maafisa katika jimbo la Nevada nchini Marekani wanachukua hatua za dharura kukabiliana na uhaba wa bangi.
Mahitaji yamekuwa ya juu tangu bangi ihalalishwe kwa matumizi ya kujiburudisha tarehe mosi mwezi huu.
Hii imetokana na ukosefu wa wauzaji wa autosha.
Sheria iliwapa wauzaji wa pombe ruhusa ya kuuza bangi lakini wengi hawatimizi mahitaja ya leseni kuweza kuuza bidhaa hizo.
Idara ya kodi katika jimbo hilo ilitangaza dharaua, inayomaanisha kuwa maafisa watachukua hatua za dharura kukabiliana na uhaba huo.

Mauzo ya karibu dola milioni 3 yalikadiriwa siku nne za kwanza baada ya matumizi ya bangi kuhalalishwa.

Nevada ilipiga kura ya kuhalalisha matumi ya bangi kwa burudani mwezi Novemba kufuatiu hatua kama hizo katika majimbo mengine.
Matumzi ya bangi kwa matibabu yameruhusiwa katika majimbo 25 ikiwemoi Nevada ambapo imehalalishwa tangu nwaka 2001.