Thursday, 18 May 2017

MEYA, WAMILIKI WA SHULE NA WAANDISHI WAKAMATWA WAKIWA SHULE YA LUCKY VINCENT

Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, wamiliki wa shule binafsi pamoja na waandishi wa habari na wadau wengine wamekamatwa na Polisi wakati wakikabidhi rambirambi na kutoa pole leo kwenye shule ya Lucky Vincent.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo ni kuwa, wageni hao waliofika shuleni hapo ambao ni pamoja na wazazi zaidi ya 20 wa watoto waliofariki katika ajali ya basi Karatu, wamiliki wa shule binafsi na wengine walioambatana nao, walichanga pesa kiasi cha shilingi milioni 28 ambazo waliamua kuzikabidhi leo kwa wahusika mmoja mmoja na si kuzikabidhi kwa mtu mwingine tofauti.
Hatua yao hiyo ilifikiwa baada yakuona kuwa michango iliyopita ilileta mkanganyiko hivyo walitaka kuhakikisha kuwa rambirambi zao zinakwenda kwa wahusika moja kwa moja lakini ghafla polisi walifika na kuwaambia kuwa walikosea kufanya mkusanyiko usio rasmi na kuwakamata.
Pamoja na hayo, waandishi pia wamekumbwa na mkasa huo kwakuwa walikwenda kufuatilia tukio hilo ambapo ni pamoja na mambo mengine lengo lao lilikuwa ni kuzungumza na uongozi wa shule pia wageni waliofika shuleni hapo wakiongozwa na Meya wa Jiji la Arusha. Waandishi waliokamatwa ni pamoja na Godfrey Thomas-Ayo TV, Alphonce Kusaga-Triple A, Filbert Rweyemamu-Mwananchi, Husein Tuta-ITV, Joseph Ngilisho-Sunrise Radio, Geofrey Steven-Radio 5, Janeth Mushi-Mtanzania, Zephania Ubwani-The Citizen, Elihuruma Yohani-Tanzania Daima na Idd Uwesu-Azam Tv .

SOURCE:MTANZANIA

0 comments:

Post a Comment