Friday, 26 May 2017

Kafulila atema nyongo baada ya Prof Muhongo Kutumbuliwa

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu David Kafulila ameibuka na kutoa ya moyoni baada ya maamuzi yaliyofanywa na Rais Magufuli baada ya kupokea ripoti ya Kamati Maalum kuhusiana na uchunguzi wa makontena 272 ya makinikia yaliyokuwa  tayari kwa kusafirishwa nje ya nchi .

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Kafulila ameandika yafuatayo,

1 Naipongeza Kamati kwa kazi iliyotukuka iliyojaa majaribu ya rushwa kubwa kwani kampuni nyingi madini, mafuta na gas duniani zina sifa hiyo kama alivyopata kusisitiza Profesa Joseph Stirglitz gwiji la uchumi na utandawazi duniani.

2 Zaidi hatua aliyo chukua Rais kuhusu uharamia huu katika sekta ya madini inapaswa kuungwa mkono na kila mzalendo kwani imekuwa hoja ya upinzani na kila mzalendo kwa miaka mingi iliyoishia kubezwa na kupuuzwa.

3 Rais asiishie kutaka uchunguzi kufanywa dhidi ya watumishi katika sekta ya madini tu, nchi hii imeoza, uchunguzi ufanywe mpaka ndani ya Idara ya Usalama na vyombo kama TAKUKURU kwani mafisadi hawa waliweka mfumo mzima mfukoni kwa kujenga mahusiano na baadhi ya wanausalama na vyombo vingine vyeti kiuchunguzi.

4 Namshauri Rais aboreshe Idara ya Usalama kwa kuwa na kitengo cha ujasusi wa kiuchumi (Economic Intelligency) kitakachoweza kumudu kukabiliana na uharamia ktk utoroshaji utajiri wa nchi (illicits flows) kwani nchi inavuja kwa miaka mingi na mtandao wa uharamia huu uliweka sehemu kubwa ya mfumo mfukoni.

5 Kuna haja yakutazama Katiba yetu upya ili ikibainika hata Rais kama alihusika na ufisadi afikishwe kwenye mkondo wa sheria kwani nchi nyingi za Africa zimeoza kwa ufisadi kuanzia Ofisi Kuu, huko ndio vinatoka VIMEMO kuruhusu uharamia wa namna hii. Ni Ushauri wangu kwa Rais aruhusu mchakato wa Katiba ili pamoja na mambo mengine tuangalie mfumo wa Ofisi Kuu kama moja ya chanzo cha uozo na uharamia huu.

6 Ni vema Mheshimiwa Rais akatambua kwamba kampuni hizi za kimataifa zinaiba duniani kote ikiwemo Ulaya na Marekani, isipokuwa huku kwetu zinaiba zaidi kutokana na sera duni, sheria dhaifu, mifumo ya usimamizi dhaifu na udhaifu wa wanaopewa nafasi kwa ujumla. Kukabili tatizo hili lazima kutazama kwa mapana na kutengeneza mfumo madhubuti.

7 Mwisho nimshauri Rais kwamba pamoja na kuchukua hatua hizi za kisheria za ndani, azifikishe kampuni hizi kwenye Mahakama za Kimataifa (Arbitration court) kama inavyo tamkwa kwenye mikataba ili kuzidai fidia kwa miaka yote ya Mikataba yao.

8 Mitambo na mali zao zishikiliwe mpaka kesi itapomalizika. Na hili lisisomeke kwamba nikukimbiza wawekezaji bali nikukabili uharamia wa utoroshaji rasilimali ambao hata sheria zakimataifa zinapiga vita. Hili ni muhimu sana. Umma una paswa kusimama pamoja dhidi ya uharamia huu!

0 comments:

Post a Comment