VITA kubwa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais Dk. John Magufuli kuanza kuchukua hatua kali dhidi ya usafirishaji wa mchanga unaodaiwa kuwa na dhahabu.
Baada ya hatua hiyo ya Rais Magufuli, kumeanza kuibuka mambo kadhaa, moja kubwa likiwa ni msafara wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Zainab Tellack kuzuiwa kuingia kukagua na kuhesabu dhahabu iliyozalishwa na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu kwa kipindi cha siku mbili, baada ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) kusimamishwa.
Zainabu, alikuwa katika ziara ya kawaida kukagua wingi za dhahabu iliyozalishwa katika migodi iliyopo mkoani kwake, baada ya Rais Magufuli kusimamisha kazi watendaji wa TMAA.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Zainabu alisema kutokana na TMAA kuondolewa, waliamua kufanya ukaguzi migodini kujua ni nini kipo na kimezalishwa wakati ili kuhakikisha usalama wa madini hayo.
Alisema alichukua uamuzi huo kuepuka udanganyifu hadi wataalamu wengine watakapopatikana kwa kazi ya ukaguzi.
“Tulifanikiwa kufika mgodi wa Buzwagi, tulikagua na kupima kiasi cha dhahabu kilichokuwapo na kuhesabu… tulipofika mgodi wa Bulyanhulu tuliingia ila hatukufunguliwa strong room (chumba cha kuhifadhia dhahabu) kama Buzwagi kwa madai wanafunga kwa muda (time lock), tulikubaliana kesho (leo), lakini nimeamua kuweka askari wa kulinda hapo mpaka kesho (leo),” alisema.
Alisema hawezi kuacha wawekezaji hao wakazalisha dhahabu bila ya kuwa na wakaguzi kama taratibu zinavyoelekeza, kwa kuwa wanaweza kuzalisha na kusafirisha wakati ambao hakuna wakaguzi.
“Labda niwaambie Watanzania, dhahabu yetu ipo salama, tumekagua na kujihakikishia walichozalisha kwa kuhesabu na kupima, waliposema hatuwezi kuingia, nimeweka ulinzi wa Serikali,” alisema.
ACACIA WAFAFANUA
Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Acacia ambayo ndiyo wamiliki wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, Nekta Foya, akizungumza na MTANZANIA jana, alisema Mkuu wa Mkoa alifika na kupokewa vyema katika mgodi wa Bulyanhulu na kupewa ushirikiano wote hadi kuingia ndani ya chumba cha dhahabu (gold room), lakini hakuingia katika sefu ya dhahabu kutokana na muda aliofika kuwa imejifunga.
“Unajua kwa ajili ya usalama, unaweza kuingia chumba cha dhahabu, usifike kwenye dhahabu kwa kuwa hufungwa kwa muda maalumu kutokana na mipango ya uzalishaji, sasa muda ambao amefika mfumo wetu wa usalama (time lock) wa sefu ya dhahabu, ulikuwa umejifunga, usingeweza kufunguka hadi kesho (leo),” alisema.
Alisema baada ya kufahamishwa na maofisa wao waliokuwapo, RC Zainabu alikubalina nao na kupanga kuendelea kesho na ukaguzi wake, lakini kutokana na kutaka uhakika zaidi aliacha askari kulinda eneo hilo.
YAPINGA RIPOTI YA KAMATI
Katika hatua nyingine, Acacia imepinga ripoti ya Kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma iliyoundwa na Rais, Magufuli kuchunguza makontena 277 yenye mchanga wa dhahabu, ikisema haikutangaza madini yote yaliyokuwa katika makanikia inayosafirisha kwenda nje ya nchi.
Ikumbukwe Rais Magufuli aliunda kamati mbili kuchunguza kiwango cha madini kilichomo katika makontena hayo ya mchanga yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda nje ya nchi kuyeyushwa kupata masalia baada ya mchakato wa kwanza kuondoa dhahabu mgodini.
Kamati hiyo iliyokabidhi ripoti yake Ikulu juzi iliongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ambaye alisema makontena yaliyozuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam yana tani 7.8 za dhahabu yenye thamani ya kati ya Sh bilioni 676 na Sh trilioni 1. 147.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Acacia, Brad Gordon, alisema kamati hiyo haikutangaza madini yote yaliyokuwa katika makanikia kwamba kutokana na hilo, amri ya kuyazuia kusafirishwa nje kubakia palepale.
“Hatukubaliani na matokeo ya tume ambayo inaeleza kuwa madini yaliyo katika mchanga uliopo katika makontena yana thamani zaidi ya mara 10 ya kiwango tulichotangaza.
“Tuna imani na usahihi wa taarifa zetu ambazo zilikaguliwa na kutathiminiwa na SGS, ambayo ni moja ya kampuni kubwa kabisa duniani za upimaji,”alisema Gordon.
Ofisa huyo wa Acacia, alisema makanikia wanayozalisha yana kiwango kidogo cha madini na kila kontena lina kiwango tofauti cha wingi wa makanikia, lakini wanaamini kila kontena lina wastani wa kilo 3,000 za shaba, tatu za dhahabu na kilo tatu za fedha.
Alisema kwa pamoja madini hayo yana thamani ya Sh milioni 300 kwa kila kontena.
“Pia tumeorodhesha kampuni huku mapato yetu yakikaguliwa kikamilifu na PWC, ambayo inathibitisha kwamba daima tuko wazi kwa kila kitu tunachofanya.
“Mapato tunayotangaza katika mahesabu yetu yaliyokaguliwa yanaendana na kiwango cha dhahabu tunachotangaza kuzalisha na kuuza.
“Iwapo kiwango cha dhahabu katika makanikia yetu kitaendana na matokeo ya tume, itamaanisha kwamba migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi inazalisha dhahabu nyingi kuliko mgodi wowote ule duniani. Kwa bahati mbaya sana uhalisia hauko hivyo.
“Nakubali kwamba wakati matukio kama ya jana yanapotokea, huleta hali ya sintofahamu na kuwafanya watu wahoji na wamwamini nani. Nataka kuwahakikishia kwamba Acacia ilitangaza kikamilifu kila kitu kwa mujibu wa thamani halisi tunayozalisha.
“Pia tunalipa mirabaha inayotakiwa na kodi kwa madini yote yanayohusika ambayo tunazalisha na kwamba usafirishaji wa makanikia hufanyika kwa mujibu wa sheria za Tanzania na makubaliano ya kisheria tuliyonayo na Serikali ya Tanzania.
“Wakati tukiwa tumesikiliza hotuba za jana (juzi) na taarifa kwa vyombo vya habari ni hadi pale tutakapopokea ripoti nzima vinginevyo ni vigumu kwetu kutoa maelezo ya kina au kutoa uamuzi kuhusu kiwango na thamani inayohusu makanikia ya Acacia kwa mujibu wa ripoti ya tume, lakini ninarudia, tunaamini juu ya kiwango tulichotangaza.
“Kuhusu mirabaha alisema Serikali hupokea mirabaha ya asilimia nne ya madini ya dhahabu, fedha na shaba iliyopo katika makanikia.
“Acacia imekuwa ikilipa mirabaha na kuna ukaguzi wa kuthibitisha hilo. Madini mengine katika makanikia hayo ni yale yasiyo na thamani katika soko kutokana na kiwango cha udogo wake na gharama za kuyachenjua huzidi thamani na hivyo hakuna mrabaha,”alisema ofisa huyo wa Acacia.
Wakati Kampuni ya Acacia ikisema hivyo, timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), ilitoa mapendekezo kadhaa kwa Serikali huku ikiitaka kuzidai kampuni zote malimbikizo ya kodi na mrabaha wa madini ambayo hazikuyataja katika taarifa zao tangu zilipoanza uchimbaji hapa nchini.
Taarifa hiyo pamoja na mambo mengine imependekeza Katiba ya nchi ifanyiwe marekebisho na kutamka wazi kuwa Tanzania ndiyo mmiliki wa milele wa rasilimali zake zote za asili.
Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT, Dk. Rugemeleza Nshala, alisema kuna mfumo mbaya wa ukaguzi na mikataba ya madini ambao unaruhusu kampuni kushiriki katika udanganyifu wa bei.
“Serikali ifute leseni za uchimbaji kwa kampuni za madini ambazo zimeshiriki katika udanganyifu huu. Tunatoa rai kwa Serikali hatua zote za kisheria za kuvunja mikataba zifuatwe kwani uzoefu wetu katika kesi ya City Water unatuasa kufuata kwa umakini taratibu za kuvunja au kusitisha mikataba.
“Iundwe idara madhubuti ya wanasheria ndani ya Serikali wanaohusika na masuala ya gesi, petroli, madini na mikataba yote ipitiwe kuona udhaifu wake,” alisema Dk Nshala.
Aidha LEAT inaishauri Serikali kushiriki katika uchimbaji wa madini kupitia kampuni zake na iwe na hisa katika kampuni mama zinazochimba madini huku ikitolea mfano nchi ya Botswana ambayo ilikuwa na asilimia 15 ya hisa katika kampuni ya ubia kati yake na De Beers.
Dk. Nshala alisema Tanzania inapaswa ijitoe katika mikataba ya usuluhishi na migogoro ya kimataifa kwani inapingana na maazimio namba 1803 ya mwaka 1962 na namba 3281 ya mwaka 1974.
Alisema migogoro yote inayohusiana na uchimbaji madini kati ya serikali na kampuni za nje za madini itatatuliwa na mahakama za ndani na si mabaraza ya usuluhishi kwa madai kuwa yalianzishwa kulinda masilahi ya kampuni za kigeni.
Kuhusu kodi, mwanasheria huyo alipendekeza sheria ya kodi irekebishwe na kuweka vifungu vya kuzuia udanganyifu wa bei na kufuta nafuu zote za uwekezaji za uchimbaji madini zilizo katika sheria ya mabadiliko ya sheria mbalimbali za fedha namba 27 ya mwaka 1997 na sheria ya mauzo ya mwaka 1976 kwani zimebariki kuporwa kwa madini.
“Yale ambayo kamati imeyabaini ni mambo ambayo LEAT ilikuwa ikiyasema kwa sauti kubwa lakini yalipokelewa kwa kejeli na uongozi wa Serikali zilizopita zikiungwa mkono na kampuni za madini kwa kuwaita wanaharakati wenye ajenda ya siri dhidi ya wawekezaji,” alisema.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo baada ya malalamiko ya wadau, Benki ya Dunia iliikopesha Serikaliya Tanzania Dola za Marekani milioni 56 kufanya mabadiliko katika Sheria ya Madini ya 1998 na kuandikwa sheria nyingine mwaka 2010.
Alisema sheria hiyo ya 2010 haina tofauti na ile ya 1998 isipokuwa kuanzishwa kwa bodi ya ushauri ya madini na waziri kuchukua nafasi ya kamati ya ushauri na kushauri ipitiwe upya.
PROFESA MOSHI
Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, akitoa maoni yake jana alisema kosa kubwa lililofanywa na Serikali ni kufungua milango ya wawekezaji katika sekta ya madini bila kuwa na uwezo wa kuwadhibiti.
“Nilitarajia ripoti itaonesha matokeo hayo na hili nililizungumza tangu mwaka 2002, kwamba mikataba mingi haipo wazi hivyo ni rahisi sana kuwa na makandokando.
“Tulifungua milango ya kukaribisha wawekezaji bila hata kuwa na uwezo wa kuwadhibiti, hili ni kosa kubwa. Wawekezaji walipewa masharti ambayo ni nafuu mno. Serikali ikutane na wawekezaji wote na wakubaliane kwamba lazima mikataba ipitiwe upya,” alisema Profesa Moshi.
PROFESA SHIVJI
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter jana akisema Serikali ilikosa njia ilipopitisha sheria ya madini mwaka 1998.
“Tulikosa njia tulipopitisha sheria ya madini ya mwaka 1998 iliyofanya mikataba iwe na nguvu zaidi kuliko sheria. Tukajifunga pingu. Nani wa kulaumu?,” alihoji Profesa Shivji.
LHRC
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema mwaka 2014, walitoa ripoti na kuiomba Serikali ichungunze na kuichukulia hatua Wakala wa Madini Tanzania (TMAA), lakini hawakusikilizwa.
“Tumeridhishwa na hatua zilizochukuliwa japo ni kwa kuchelewa. Mwaka 2014 tulitoa ripoti yetu na maoni yetu kuhusu mikataba ya madini na tukaiomba Serikali iichunguze TMAA lakini hawakutusikiliza ni wakati sasa wa kupitia upya mikataba yote ya madini,”alisema Henga.
CCM: Rais akaze buti
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Humphrey Polepole alisema kwamba Rais Magufuli anapaswa kuungwa mkono kwa sababu vita hii ya uchumi aliyoingia ni ngumu kuliko ile ya kutumia silaha.
Watanzania kwa pamoja wanapaswa kuungana ili kuhakikisha kuwa viongozi au watu wanaohujumu uchumi wa nchi wanakomeshwa na kuchukuliwa hatua.
Wakati huo huo Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) umeishauri serikali kupitia upya mikataba yote ya madini ili kubaini kama ina manufaa kwa taifa ama laa.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka wakati akitoa tamko la umoja huo jana alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli kuzuia utoroshaji wa madini lakini pia kama kuna viongozi waliohusika wachunguzwe mali zao na ikibidi zitaifishwe.
“Tumeishauri serikali kutaifisha mali za viongozi na watendaji ambao watabainika kumiliki mali, utajiri, na vitega uchumi ambavyo havilingani na vipato vyao kama ilivyofanyika mwaka 1967 baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha ,” alisema Shaka.
source:mtanzania
0 comments:
Post a Comment