Friday 26 May 2017

Hatimaye simu mpya za Nokia 3310 zaingia madukani

 Simu hizo mpya za Nokia 3310 zitakaa muda mrefu na chaji kuliko simu asili

Simu za Nokia 3310 zimeanza kuuzwa tena madukani, takriban miaka 17 baada ya simu hizo kuanza kuuzwa mara ya kwanza.

Simu za sasa zina kamera ya megapikseli mbili na zinategemea teknolojia ya 2.5G kumpa mteja huduma ya kiwango cha chini sana cha mtandao wa Intaneti.

Simu hiyo inauzwa £49.99 (Dola 65).

Betri za simu hizo zinadaiwa kudumu kwa saa 22 mtu akiitumia kuzungumza, na inaweza kukaa na chaji kwa hadi mwezi mmoja iwapo mtu hatakuwa anaitumia.

Mtaalamu mmoja amesema ufanisi wa simu hiyo utategemea sana hamu ya watu kutaka kulipia kifaa hicho ambacho wengi bado hukikumbuka kwa mazuri yake.

Watu wengi walizipenda sana simu za Nokia 3310 kutokana na uthabiti wake na uwezo wa kukaa na chaji.

"Kwa mtu kama mimi, siku ya leo ni ya furaha sana," alisema Ben Wood, kutoka kwa kampuni ya masuala ya teknolojia ya CCS Insight.

"Ukiweka simu hii mikononi mwa mtu aliyebalehe karne ya 21 ambaye uraibu wake ni kukaa Snapchat, bila shaka utakuwa umekosea.

"Ikizingatiwa kwamba kuna zaidi ya simu 20 milioni za rununu Uingereza, na takriban simu milioni moja za msingi, au 'simu za zamani' ukitaka kuziita hivyo. Inaonekana bado kuna soko.

Mchezo wa Snake pia umeboreshwa

"Simu hii ni ya kiwango cha juu kidogo, kwa hivyo, swali ni watu wako tayari kuilipia pesa ngapi?"

Simu asili za Nokia 3310 zilipendwa sana kwa kuwa thabiti na kukaa muda mrefu na chaji

Mwanblogu wa anayepakia video zake Youtube Safwan Ahmedia alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kununua simu hizo.

Msemaji wa kampuni ya Vodafone ameambia BBC: "Tuna furaha sana kuwa na simu hizi kwani watu wengi wanazitaka wazinunue."

Sifa za Nokia 3310

Uzani 79.6g

Mfumo endeshi Nokia S30+

Mtandao 2.5G, Bluetooth 3.0

Kamera Megapikseli mbili

Uhifadhi wa data 32MB, microSD hadi 32GB

Betri Muda ambao mtu anaweza kuongeza bila betri kuisha chaji ni saa 22, bila kutumia simu chaji inaweza kudumu mwezi mmoja

Bei £49.99

Habari kuwa simu hiyo ingeanza kuuzwa tena Februari wakati wa maonesho ya kila mwaka ya teknolojia ya simu za rununu mjini Barcelona.

Simu za sasa zinaundwa na kampuni ya HMD Global ya Finland ambayo ilipewa leseni ya kuunda simu hiyo. Kampuni hiyo imekuwa pia ikiunda simu kadha za kisasa za Nokia zinazotumia mfumo endeshi wa Android.

Nokia ilitengeneza simu zaidi ya 126 milioni asili za 3310 kati ya 200 na 2005 kabla ya kuacha kuziunda tena.

Kampuni hiyo haijaunda simu za rununu tena tangu ilipounza biashara yake ya simu kwa Microsoft mwaka 2013.


0 comments:

Post a Comment