JESHI la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia Pastory Chilangazi (37), mkazi wa Kijiji cha Mamvisi, Wilaya ya Gairo kwa tuhuma za kumuua mkewe kwa kipigo kutokana na kile kinachoelezwa ni kutofautiana baada ya mkewe huyo kudai fedha za matibabu ya mtoto wao.
Ilielezwa zaidi kuwa baada ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa aliutupa mwili wa mkewe mtoni.
Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema tukio hilo lilitokea Mei 22, majira ya asubuhi.
Kamanda Matei alisema mwanaume huyo alimpiga ngumi na mateke mkewe, Edina Mazengo (32), katika sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo kabla ya kwenda kuutupa mwili wake katika Mto Chumvi.
“Taarifa tulizopata huko ni kwamba mwanamke huyo alimwomba mumewe fedha za kumpeleka mtoto hospitalini.
Hapo ndipo kulipotokea vurugu na mwanaume kuanza kumpiga mke wake hadi kumsababishia umauti,” alisema Kamanda Matei, akimtaja mtoto wa wawili hao aliyekuwa akitakiwa kupelekwa hospitalini kuwa ni Emmanuel Pastory (4).
Alisema tayari mtuhumiwa ameshakamatwa na polisi na anaendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
source:muungwana
0 comments:
Post a Comment