Friday 26 May 2017

Neema Ajira zaidi za 250 Wizara ya Ardhi


SERIKALI imezidi kutangaza neema ya ajira kwa Watanzania baada ya kubainisha kuwa katika mwaka ujao wa fedha watumishi wapya 291 wataajiriwa katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi, aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana alipokuwa akiwasilisha hotuba yake kuhusu utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha na makadirio ya mapato na matumizi yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Mbali na ajira hizo mpya, alisema wizara yake itatoa mafunzo kwa watumishi 70 na kuboresha ofisi zake ili kuwezesha watumishi wengi zaidi kuhamia Dodoma.

Changamoto Tano
Lukuvi alisema wizara hiyo inakabiliwa na changamoto tano ambazo ni pamoja na uratibu wa sekta ya ardhi kusimamiwa na mamlaka zaidi ya moja na upungufu wa wataalamu na vitendea kazi vinavyohitajika ili kukidhi utoaji wa huduma katika sekta ya ardhi.

Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni kasi ya ongezeko la watu na mifugo kulinganishwa na upatikanaji wa ardhi iliyopangwa na kupimwa, ucheleweshaji wa ulipaji wa fidia stahiki kwa ardhi iliyotwaliwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu sera na sheria za nchi.

Ili kutekeleza majukumu yake katika mwaka ujao wa fedha, Lukuvi aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya jumla ya Sh. bilioni 70.77. Kati yake, Sh. bilioni 25.4 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh. bilioni 61.873 kwa ajili ya bajeti yake ya mwaka huu wa fedha. Kati yake, Sh. bilioni 20 zilikuwa za maendeleo.

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya wizara hiyo, Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wilfred Lwakatare, aliishauri serikali kumaliza changamoto ya migogoro ya ardhi nchini, kuitaka Mamlaka ya Mapato (TRA) kuongeza kasi ya makusanyo ya kodi ya majengo na kuhamisha ajira za sekta ya ardhi kutoka serikali za mitaa kwenda serikali kuu.

Lwakatare ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), aliishauri serikali kuunda mamlaka ya kusimamia sekta ya miliki hasa za majengo makubwa, kuwafidia wananchi waliobomolewa nyumba kupisha miradi ya serikali, kutathmini gharama za nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba (NHC) na kuwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kutoingilia majukumu ya mabaraza ya ardhi.

source:muungwana

0 comments:

Post a Comment