Tuesday, 30 May 2017

Mume amuua mkewe kwa kipigo

Mwanamke mmoja amekutwa akiwa amefariki dunia chumbani kwake huku mwili wake ukiwa na majeraha baada ya kupigwa na mumewe, wilayani ilemela mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amesema kwamba tukio hilo limetokea leo tarehe 30, Mei 2015 saa 9:09 alfajiri katika mtaa wa Pasiansi Mashariki wilayani humo.

Kamanda Msangi amesema tukio hilo limetokea baada ya kuzuka kwa ugomvi kati yao ambapo mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Ester Charles (30)  alipigwa na mumewe na baadaye mwanamume huyo anayefahamika kwa jina la Charles John (35) kutoroka kusiko julikana.

Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa akiishi nyumbani kwao na mumewe lakini kwa kipindi chote wakiwa kwenye mahusiano  wawili hao walikuwa kwenye migogoro ya mara kwa mara ya ndani ya familia kwani mwanamke alikuwa akimtuhumu mumewake kwamba anatoka nje ya ndoa.

JINSI ILIVYOKUWA
Inasemekana kuwa usiku huo majirani walisikia ugomvi ukiendelea kati ya wawili hao huku mwanamke akipiga kelele akiomba msaada, lakini majirani hawakwenda kuwasaidia kwani walizoea kuwasikia wakipigana na baadaye kuelewana kisha kuendelea na maisha kama kawaida.

Baada ya muda kupita hapakusikika tena ugomvi hivyo majirani walijua tayari wameelewana, lakini baadaye alisikika mtoto akilia kwa muda mrefu ndipo walipata mashaka kisha walitoa taarifa kituo cha polisi.

Polisi walifika eneo la tukio kisha kumkuta mwanamke huyo akiwa tayari amepoteza maisha, huku mwili wake ukiwa na majeraha ya kupigwa na kitu kizito maeneo mbalimbali ya mwili wake na shingoni kwake kukionekana kukabwa na kitambaa kigumu na mumewe aliyekuwa wakipigana kisha baada ya kuona mkewe amefariki dunia alitoroka kusiko julikana.

Amesema polisi wapo kwenye msako mkali wa kuhakikisha mtuhumiwa wa mauji hayo anakamtwa, huku upelelezi ukiwa unaendelea.

source:muungwana

0 comments:

Post a Comment