Thursday, 25 May 2017

Wajumbe wa kamati Iliyomng'oa Muhongo walitishwa

RAIS Dk. John Magufuli amebainisha kuwa licha ya kamati ya Kuchunguza Makontena ya Mchanga wenye Madini (makinikia) kupewa ulinzi mkali, kulikuwapo vitisho na hata baadhi ya wajumbe kutaka kuhongwa.

Akizungumza jana wakati wa kukabidhiwa ripoti ya uchunguzi na kamati hiyo, Rais Magufuli alisema vilijitokeza vitisho na watu kuzungumza kwa lengo la kupotosha huku ikionyesha kuwa wamelipwa fedha kufanya hivyo.

 “Tulitumia vifaa vyote vinavyowezekana katika ulinzi, pamoja na hatua hizo wapo waliojitokeza kutaka kuingilia uchunguzi huu. Kwa bahati nzuri majina yao tunayo, wapo waliojitokeza hadharani baada ya kupewa fedha. Kuna mtu anajiitaga Profesa wakati ni Daktari alihongwa fedha mbele ya kamera,” alisema na kuongeza:

“Akaanza kuzungumza ambayo hayajui, nimesikia wengi wakibwatuka wengine kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu ya jeuri ya fedha walizopewa. Hatuna ushahidi ila ukishaona mtu anabwatuka kwa suala la maslahi ya taifa, hafanyi bure bali kuna kitu kimempa kiki.”

Rais alisema Watanzania wanatakiwa kutambua kuwa nchi iko kwenye vita ya uchumi ambayo ni mbaya sana.

Alisema mabilioni ya fedha yaliyopotea ni dhahabu tani 7.8 hadi 13.16 kwa makontena 277, ambazo kwa mujibu wa Rais, ni sawa na tani 15.5 za dhahabu ambazo kwa lugha rahisi ni sawa na malori mawili ya tani saba na landrover moja ya tani moja.

 “Hii ni kwa makontena 277, ninajua kuna Tume itatueleza ni makontena mangapi yaliyosafirishwa, ila ninachojua wanasafirisha makontena 250 na zaidi ya 300 kwa mwezi, kwa mwaka ni zaidi ya makontena 3,600 maana yake ni tani 171 hadi 200 za dhahabu, ukizidisha kwa miaka 17 utajua ni tani kiasi gani na trilioni kiasi gani, hii ndiyo Tanzania,” alisema.

“Tunasubiri kamati nyingine itakuja na hesabu kamili na hapo ndipo ripoti yote ya wataalamu itakuwa imekamilika, hiki ni kitu cha kuumiza mno, ni aibu sana, nilifikiri katika hili Watanzania tushikamane.

“Unapoenda kwenye hospitali watu wanakosa dawa, vitanda, mashuka, madarasa hayatoshi, madawati lazima tuchangishane, miundombinu tunahangaika kutafuta hela za kujenga treni mpaka tukope, tujibane, kumbe kuna hela zinamwagika hapa,” alisema.

“Wapo Watanzania tuliwapa wajibu wa kusimamia, hawajali na hilo linauma sana!”

0 comments:

Post a Comment