Wednesday, 31 May 2017

Kambi ya Upinzani Bungeni uvunjwe

MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema), amelitaka Bunge kuvunja Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutokana na maoni ya kambi hiyo kutosikilizwa.
Lema amedai kuna kuchujwa kwa maneno yanayochangiwa na wabunge wa kambi hiyo katika mijadala katika taarifa za kumbukumbu za Bunge(hansard), alikodai kunafanywa na wafanyakazi wa Studio ya Bunge.

Aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana asubuhi aliposimama na kuomba mwongozo wa Kiti cha Spika akidai kuwa michango ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikihaririwa na baadhi ya maneno yamekuwa yakiondolewa na hivyo kutorushwa kwenye studio hiyo na hata kwenye taarifa wanazopewa waandishi wa habari wa redio na televisheni.

Hata hivyo, katika mwongozo wake kuhusu suala hilo muda mfupi kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge jana mchana, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga, aliyekuwa akiongoza kikao cha jana, alisema Studio ya Bunge haina utaratibu wa kuchuja michango ya wapinzani isipokuwa kwa maelekezo ya Kiti cha Spika.

Katika hoja yake, Lema alisema ni bora Bunge lingetoa mwongozo wa kuivunja Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na lisipokee tena maoni yoyote kutoka kwao kutokana na maoni yao kutosikilizwa.

"Mwongozo wangu Mheshimiwa Mwenyekiti kupitia Kanuni ya 68(7) cha jambo lilotokea jana (juzi) jioni, michango ya wabunge tunayochangia humu ndani ni rekodi ya wabunge kama ambayo inavyoingia katika ‘Hansard’ na ni rekodi kwa matumizi yetu binafsi," alisema.

Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi huyo alisema zaidi: "Lakini baadhi ya michango yetu ukifuatilia kule ambako inahifadhiwa kama kumbukumbu zetu binafsi kwa matumizi yetu, Mheshimiwa 'wana-edit' (wanahariri) kwa zaidi ya asilimia 70 na wanaweka mambo ambayo wanayataka wao.

"Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimechangia Wizara ya Mambo ya Nje na (Ushirikiano wa) Afrika Mashariki, nikaenda nikaambiwa nijaze fomu, nimejaza kutaka kumbukumbu ya mchango wangu, mchango ambao haukuwa hata na mwongozo, haukuwa na taarifa wala utaratibu (bungeni).

"Nimekwenda mambo yote yanayohusu mambo ya Acacia na Diplomasia ya Uchumi yametolewa, wamenibakizia pale panaposema tu kupinga na mtu yoyote anayepinga rasilimali ni mwendawazimu na kipande hicho ndiyo kinazungushwa.

"Sasa Mheshimiwa Mwenyekiti, michango yetu hapa bungeni ni kumbukumbu zetu na hili Bunge Mheshimiwa Mwenyekiti, limeondolewa kuwa 'live' (matangazo ya moja kwa moja) na uhuru wake umeminywa halafu michango yetu ambayo ni halali tukiifuatilia kwa kumbukumbu zetu 'mna-edit'.

"Sasa Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bora Bunge hili likatoa mwongozo wa kuvunja Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na msipokee maono yoyote kutoka kwetu."
Awali akijibu mwongozo huo asubuhi, Giga alisema angefuatilia kama madai ya Lema yana ukweli au la na baadaye kutoa majibu bungeni.

"Ni kwamba michango ambayo tunachangia kwa maandishi tunaletewa kwanza hapa kwa ajili ya kuweza kurekebisha lakini kama ni ‘clip’, basi hili suala itabidi nilifuatilie kwa sababu sina uhakika nalo kama ni kweli au siyo kweli, baadaye tutaweza kuleta majibu yangu. Huo ndiyo mwongozo wangu," alisema Giga.

Ndipo kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge mchana, Mwenyekiti wa Bunge huyo alisema amefuatilia na kupata maelekezo kwamba studio ya chombo hicho cha kutunga sheria na Ofisi ya Bunge kwa ujumla hawana utaratibu wa kuchuja michango ya wabunge isipokuwa tu kwa maelekezo ya Kiti cha Spika yanayotolewa bungeni.

Alisema taarifa zinazokuwa kwenye 'hansard' zinapaswa kuwiana na 'clip' za mchango wa mbunge husika.

"Kilichotokea kwa mchango wa Mheshimiwa Lema ni kosa la kiufundi na linafanyiwa kazi na likitatuliwa, anaweza kuomba na kupewa mchango wake wote," alisema.

Giga aliongeza kuwa mbunge yeyote atayekumbana na changamoto kama iliyompata Lema, awasilishe malalamiko yake kwenye Ofisi ya Katibu wa Bunge.

0 comments:

Post a Comment