Friday, 26 May 2017

LOWASSA, LIPUMBA WAGONGANA MSIBANI


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba wamekutana ana kwa ana kwenye mazishi ya mwanasiasa mkongwe na Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Kitwana Kondo (KK) aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 92.
Mazishi hayo yalifanyika jana na aliyekuwa wa kwanza kufika nyumbani kwa marehemu Upanga, alikuwa Profesa Lipumba, ambapo baada ya muda aliingia Lowassa na kuamua kwenda kukaa kiti cha nyuma.

Tukio hilo liliwakutanisha wanasiasa hao ambao waliachana Julai 21, mwaka 2015 wakati wa harakati za Uchaguzi Mkuu baada ya Lowassa kujiunga na Chadema na kuridhiwa kuwa mgombea urais wa chama hicho na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hata hivyo baada ya swala ya maiti, Lipumba alimfuta Lowassa na kwenda kumsalimia huku waombolezaji waliofika msibani hapo wakibaki kuwaangalia wanasiasa hao ambao sasa wamekuwa wakirushiana maneno.
Baada ya kusalimiana na kukaa pamoja wanasiasa hao wakati wakijiandaa kuelekea msikitini na kisha katika makaburi ya Tambaza,  Prof. Lipumba alionekana kila wakati akizungumza na Lowassa pamoja na mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru.
Viongozi wengine waliokuwapo msibani hapo ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Alli Hassan Mwinyi, Waziri wa zamani wa Ulinzi, Edger Majogo, Kingunge Ngombale Mwiru, Balozi Juma Mwapachu na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdurhman Kinana.
Wabunge wa zamani wa Kinondoni, Peter Kabisa na Idd Azzan, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Meya wa zamani Kinondoni,  Salum Londa, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Adam Kimbisa.
Alhaji Mwinyi
Rais Mstaafu Alhaji Hassan Mwinyi,  alisema marehemu Kitwana Kondo, alikuwa mtu mwema, mcheshi na mwenye roho ya kipekee kiasi cha kwamba hata mtu akiwa na dhiki ya rohoni akifika kwake ni lazima atapoa.
“Ni mkweli hapendi kudanganya mtu na hata kama ana njaa hawezi kukaa kimya anafika ofisini kwako na kukwambia naomba kazi yoyote nipate fedha nile,’’ alisema Rais Mwinyi.
Lowassa
Kwa upande wake Lowassa alisema Kitwana Kondo alishirikiana naye katika mambo mengi hasa ya kiserikali katika kujenga nchi. “Alikuwa mcheshi mwenye kupenda kila mtu,” alisema.
Lowassa alimwomba Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita kutenga barabara moja na kuiita jina la Kitwana Kondo ‘KK’.
Kwa upande wake Kingunge alisema marehemu alikuwa rafiki yake na kaka yake pia walijuana miaka mingi na kwamba amefanya mengi kwa ajili ya wakazi wa Dar es Salaam.
Kinana
Katibu Mkuu wa CCM , Abdulrahman Kinana alisema Kitwana Kondo,  alikuwa ni zaidi ya kiongozi wa wakazi wa Dar es Salaam na aliyejaaliwa uungwana.
“Alikuwa ni mtu aliyejaaliwa uungwana maarifa  na lugha nzuri asiyependa maneno maneno ya kusema sema, bingwa wa Kiswahili kizuri na alifanikiwa kufanya kazi na Serikali katika awamu mbalimbali,’’ Kinana.
Awali aliyewahi kuwa Mbunge wa Kisarawe, Athuman Janguo,  alisoma wasifu wa Kitwana Kondo  na kusema kuwa ameshinda nafasi mbalimbali ikiwemo kuwa Inspekta wa Jeshi la Polisi na aliyefanya kazi kwa weledi.
Alisema aliwahi kuwa Mbunge wa Kigamboni na pia aliwahi kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
“Kabla ya nafasi hizo aliwahi kupitia sehemu mbalimbali ikiwemo bodi ya Korosho, Bandari na maeneo mengine mbalimbali,’’ alisema.
Janguo alisema marehumu Kitwana Kondo, alianza kuugua mwaka 2013 kwa kusumbuliwa na shinikizo la damu  na baadaye kupata ugonjwa wa kiharusi kwa muda wa miaka mine ambapo alikuwa mahututi hadi mauti yalipomkuta juzi.

0 comments:

Post a Comment