BAADHI ya wabunge wamelalamikia vitendo vinavyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii, kukamata na kupiga mnada mifugo inayoingia kwenye hifadhi za taifa.
Kutokana na vitendo hivyo, watunga sheria hao wameishauri serikali kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wafugaji ili kuendeleza sekta ya mifugo nchini.
Waliyasema hayo bungeni mjini hapa juzi na jana wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka ujao wa fedha.
Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka (CCM), akiwa na nyaraka zinazoonyesha uongozi wa juu wa nchi ulizuia kuwaondoa wafugaji kwenye hifadhi za Mkoa wa Kagera, alisema ameshangazwa na kitendo cha maofisa na askari wanyamapori kukamata mifugo mkoani humo na kuipiga mnada.
"Haiwezekani maeneo mengi yanaendelea kuwa hifadhi wakati Watanzania hawana pa kulima," alisema Prof. Tibaijuka.
Waziri huyo wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza: "Makamu wa Rais ambaye tunajivunia sana sisi kina mama, aliandika barua rasmi kwamba mifugo iendelee kuwa ilipo mpaka utakapotolewa ufafanuzi mpya wa serikali.
"Oktoba 11, 2016, Waziri (wa Maliasili na Utalii) akatoa tamko hapa akasema kutokana na uamuzi wa ngazi za juu serikalini, wananchi na mifugo ibaki hapo ilipo.
"Sasa kilichotokea, kamati iliyoundwa imewaondoa wananchi. Huwezi kusema unasaidia kilimo wakati mifugo inatolewa kwenye hifadhi. Wafugaji sasa wanaenda kumaliza mazao yote. Inakuwaje hivi vitu vinatushinda wakati tunakwenda kujenga 'standard gauge' (reli ya kisasa)?" Alihoji Tibaijuka huku akionyesha nyaraka nane za matamko na barua mbalimbali za viongozi wa serikali.
"Kama yote haya hayatoki, wafugaji wameporwa ng'ombe wao kwenye mapori. Msimamo wangu, na nyaraka zote hizi za uwasilishaji wangu wa kiprofesa, suala hili ni la usalama wa taifa. Ng'ombe 2000 wameporwa maporini. Wanauziana wao kwa wao. 'It is totally unacceptable' (haikubariki)."
Alidai maofisa wa maliasili wanauziana wao kwa wao ng'ombe wa wafugaji kwa bei nafuu huku akiitaka wizara ithibitishe imewauza ng'ombe hao kwa watu wote kama maofisa wake hawajauziana wao kwa wao.
Aliishauri serikali kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji nchini kama ambavyo Rwanda imefanya kwa wafugaji wake.
Mbali na Tibaijuka, wabunge wengine waliochangia hoja hiyo ni pamoja na Gibson Meiseyeki (Arumeru Magharibi - Chadema) ambaye aliitaka serikali kueleza bungeni hatua ilizozichukua dhidi ya askari waliowaua wafugaji watano jimboni kwake kwa kuwapiga risasi mwanzoni mwa mwaka huu.
Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku (CCM), aliliambia Bunge kuwa hawezi kumuunga mkono Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe hata siku moja kama hajabadilika.
Alisema wananchi wanaoishi vijijini hususan pembeni mwa mapori ya hifadhi wanapata shida kutokana na askari wa maliasili.
"Maliasili wamejaza baiskeli za watu waliokamatwa na gunia la mkaa. Ng'ombe wa Wasukuma wamekamatwa, lakini wa Wanyarwanda wanaambiwa watoe. Mnada wa ajabu umefanyika, ng'ombe 500 wanauzwa Sh. milioni 300, wanauziana wao kwa wao," alisema.
"Ninyi mmesoma, lakini hamjui uchungu wetu sisi wafugaji wa ng'ombe. Sitaunga mkono kabisa hoja yako Mheshimiwa Maghembe," alisema.
Edwin Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini (CCM), aliishauri serikali kuwekeza katika utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa wananchi ili kutatua changamoto ya migogoro iliyopo kati ya jamii na mamlaka za uhifadhi, ushauri ambao pia uliungwa mkono na Joseph Kakunda (Sikonge-CCM), Haji Mponda (Malinyi-CCM) na Josephine Genzabuke (Viti Maalum -CCM).
0 comments:
Post a Comment