Wednesday 31 May 2017

Simba yapania Kumsajili Aishi Manula na kumtema Agyei


SIMBA inataka kumuacha kipa Mghana, Daniel Agyei ili imsajili kipa wa Azam FC, Aishi Manula.
Na hiyo ni kufuatia habari za Aishi kutokubaliana na Azam kuongeza mkataba, baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa sasa mwezi ujao.

Uongozi wa Simba SC unaamini ukimpata Aishi hautakuwa na sababu ya kuingia gharama za ziada kwa kuendelea kuwa na kipa wa kigeni, Agyei aliyejiunga na Wekundu hao wa Msimbazi Desemba mwaka jana kutoka Medeama SC ya Ghana.

Hata hivyo, wazo hilo linapingwa na baadhi ya viongozi wa Simba, wanaoamini Agyei ni bora zaidi ya Aishi na ndiye anayeIfaa klabu hIyo kwa sasa ikirejea kwenye michuano ya Afrika.

Simba ilikata tena tiketi ya kurudi kwenye michuano ya Afrika, baada ya kutwaa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza Uwanja wa Jamhuri Dodoma Jumamosi iliyopita.

Na kwa ushindi huo, Simba imekata tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani na pia itafungua msimu ujao kwa kumenyana na mahasimu, Yanga SC katika mechi ya Ngao ya Jamii. 

Simba ilicheza michuano ya Afrika kwa mara ya mwisho, mwaka 2013 na kutolewa na Recreativo de Lobolo ya Angola Raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa vipigo vya nyumbani na ugenini, ikifungwa 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na 4-0 ugenini.

Na Agyei ameidakia Simba jumla ya mechi 25 za mashindano yote, akifungwa mabao 10 huku mechi 16 akidaka bila kuruhusu nyavu zake kuguswa.

Alisajiliwa kuchukua nafasi ya kipa Muivory Coast, Vincent Angban ambaye naye pia aliachwa akiwa ana rekodi nzuri.

0 comments:

Post a Comment