Friday, 26 May 2017

MADIWANI WANNE CCM WATUMBULIWA


Na Ibrahim Yassin – KYELA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimewasimamisha uanachama madiwani wake wanne wilayani Kyela huku 14 wakipewa onyo kali kwa kuhusishwa na usaliti.
Akizungumza   na gazeti hili kwa simu jana, Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Wilson Nkambaku, alisema uamuzi huo umetokana na kikao cha Kamati ya Siasa mkoa kilichoketi Mei 22, mwaka huu.

  Katibu huyo alisema mchakato   bado unaendelea I kukamilisha hatua hizo zilizochukuliwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM toleo la mwaka 2012 Ibara ya 93 kifungu kidogo cha 93.
“Kusimamishwa au kuvuliwa uanachama ni adhabu ndani ya chama kwa mujibu wa kanuni za maadili toleo la 2012 ibara ya 8, ambayo inasema kosa kubwa kuliko yote ndani ya chama ni kusaliti, hivyo yeyote atakayefanya kosa hilo lazima afukuzwe,” alifafanua Nkambaku.
  Katibu wa CCM Wilaya ya Kyela, Christina Kibiki, alithibitisha kupokea barua hiyo na kwamba tayari wahusika wote wamepewa barua zao huku Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri akipewa nakala ya barua hiyo.
 “Kazi yangu mimi ni kuhakikisha wahusika wote wamepewa barua zao kutokana  na kile kilichoamuliwa katika ngazi za juu.
“Hivi ninavyokueleza, na uzuri wake  wahusika wote wamepokea rasmi barua zao kwa kusaini kitabu cha kukiri kupokea,” alisema Kibiki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmauri hiyo, Mussa Mgatta, alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, hakujibu chochote.
Kwa mujibu wa nakala ya barua hiyo yenye kumbukumbu namba CCM/KYL/MMW/30/118 ya Mei 22 mwaka huu, ambayo gazeti hili liliipata, madiwani hao wamesimamishwa kutokana na makosa matatu.
Barua hiyo imeorodhesha makosa hayo kuwa ni: Usaliti ambao inadaiwa walishirikiana na Chadema kwa lengo la kukigawa chama, kugoma kuhojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili   kugoma kuhudhuria kikao cha pamoja cha kamati ya siasa ya mkoa kilichofanyika Mei 13, mwaka huu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa barua hiyo, madiwani wengine 14, kati hao wa kata saba na viti maalumu saba, wamepewa adhabu ya onyo kali kufuatiliwa nyendo zao kwa  miezi 12 na kutakiwa kutofanya kosa lolote.
Chanzo cha madiwani hao kusimamishwa ni hatua ya madiwani 19 kutoka CCM wakishirikiana na wenzao 12 wa Chadema na kumwandikia barua mkurugenzi wa wa halmashauri wakimtaka kuitisha kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani kwa lengo la kumng’oa mwenyekiti wa halmashauri baada ya kukosa imani naye.
Mwenyekiti huyo alihusishwa na tuhuma lukuki ikiwamo ubadhirifu wa Sh milioni 700 hali iliyosababisha kuundwa   Tume ya Uchunguzi na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla,   kufanya uchunguzi wa fedha hizo.
M mmoja wa madiwani waliosimamishwa, Lameck Mwambafula wa Kata ya Bujonde, alikiri kupokea barua hiyo akisema hana pingamizi na uamuzi huo,   akihoji kanuni zililotumika kufikia uamuzi huo huku hatima yao ikibaki mbele ya Kamati Kuu ya CCM.
SOURCE:MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment