SERIKALI imesema hakuna sheria yoyote inayowapa haki wanajeshi kutesa raia au kuvunja sheria.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Magereli (Chadema), ambaye alitaka kujua sheria ipi inayowapa wanajeshi haki ya kutesa raia.
Pia mbunge huyo alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani kukomesha hali hiyo.
Alisema askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na hata Jeshi la Polisi, wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kutesa raia.
“Matukio haya yamekuwa yakitokea maeneo ya sherehe, kwenye foleni za magari, mitaani na katika magari ya usafiri wa umma. Hivi karibuni mkoani Tanga, kondakta wa daladala alimzuia mtoto wa mwanajeshi kupanda daladala yake bila nauli, matokeo yake kijana huyo alikamatwa na kuteswa na wanajeshi ndani ya kambi kitu kilichosababisha kifo chake,” alisema mbunge huyo.
Dk. Mwinyi alisema matukio ya wanajeshi kutesa na kushambulia yamekuwa yakijitokeza katika mazingira yanayohusisha kutofautiana kauli, ulevi, wivu wa kimapenzi na hata ujambazi.
“Hivyo katika kushughulikia hali hii, mara nyingi kesi hufunguliwa kwenye mahakama za kiraia na hukumu kutolewa kwa mujibu wa sheria zilizopo hapa nchini,” alisema Dk. Mwinyi.
0 comments:
Post a Comment