Friday 26 May 2017

Taarifa Muhimu kutoka Idara ya Elimu Chalinze Mkoani Pwani


IDARA ya elimu Halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani imeishukuru Serikali Kuu kwa kuwapatia vitabu 109, 673 vyenye thamani ya zaidi ya sh. Mil. 117.

Afisa elimu Halmashauri hiyo Bi. Zainabu Makwinya alisema kwamba, vitabu hivyo ni vya elimu ya msingi na sekondari ambavyo vimegawanyika sehemu kuu tatu, 95, 819 vya shule za msingi, 10, 603 vya sekondari masomo ya sanaa kidato cha 1 mpaka cha 4 huku vitabu 3,251 vya masomo ya sayansi.

"Tunaishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania na Waziri mwenye dhamana Profesa Joyce Ndalichako kwa kuona umhuhimu wa kutupatia vitabu hivyo vinavyolenga kuboresha taaluma katika Halmashauri yetu, tumevipokea kisha kuvisambaza maeneo husika," alisema Makwinya.

Akizungumzia idadi ya shule kwa mfumo rasmi, alisema kwamba kuna shule za msingi 111, kati ya hizo 6 zina umiliki wa watu binafsi, huku 105 zikimilikiwa na Serikali, pia kuna vituo vya elimu ya awali 110, miongoni mwa hivyo 105 vya Serikali vilivyosalia vya watu binafsi.

"Halmashauri yetu imefanikiwa kuwa na shule zipatazo 21 za Sekondari, kati ya hizo za watu binafsi 4, zilizosalia 17 za Serikali, aidha kuna Chuo kimoja Cha Ualimu, shule hizo 21 zina kidato cha 1-4, pia 4 kati ya hizo zina kidato cha 5 na 6 kwa mwaka huu wa 2017," alisema Ofisa huyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Said Zikatimu alisema, Serikali imeshatimiza wajibu wake wa kuipatia idara hiyo vitabu hivyo kwa ajili ya masomo hayo, kilichobaki kwa walimu kutimiza wajibu wao wa kufundisha kwa bidii ili wanafunzi wapate kile walichokidhamilia binafsi na serikali yao.

"Imani yangu ni kwamba walimu watatekeleza majukumu yao ipasavyo ya kuwapatia vijana wetu mafundisho yatayozingatia vigezo vyote ili mwisho wa siku walengwa hao waweze kukidhi kusimamia viwanda vinavyojengwa ndani ya Halmashauri, wilaya ya Bagamoyo, Mkoa na nchi kwa ujumla," alisema Zikatimu.

source:muungwana

0 comments:

Post a Comment