Friday 26 May 2017

Adhabu kali kwa Raia Wanaoishi bila ndoa Burundi

Pierre-Nkurunziza Rais wa Burundi
Watu wanaoishi katika mahusiano ya mume na mke bila kufunga ndoa nchini Burundi wameamrishwa kwamba wawe wameoana rasmi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu la sivyo wataaadhibiwa vikali.

Msemaji wa Wizara ya mambo ya ndani na elimu Terence Ntahiraja amesema amri hiyo itasaidia kile alichokitaja kuwa ni ongezeko la watu nchini Burundi.

Amesema mahusiano yasiyo rasmi yamesababisha wasichana wengi wa shule kupata ujauzito na wanaume kupata fursa ya kuwa na mahusiano ya wanawake wengi kwa mkupuo.

Rais Pierre Nkurunziza, ambaye ni muumini wa kilokole , hivi karibuni alianzisha kampeni ya kitaifa ya maadili mema.

Waziri Ntarihaja ameambia AFP kwamba ndoa zilizorasmishwa kanisani au katika afisi ya serikali ndiyo suluhu pekee kwa tatizo la ongezeko kubwa la watu nchini humo na kwamba ni jukumu la kizalendo.

"Tunawataka raia wa Burundi wafahamu kwamba kila mtu anawajibikia maisha yake, na tunataka utulivu na utawala wa sheria humu nchini," alisema.

"Juhudi zote zinafanywa kwa kufuata mkakati wa kuwafunza raia wawe wazalendo," alisema, akirejelea mpango huo wa kueneza uzalendo uliozinduliwa na Rais Nkurunziza.

Haijabainika ni adhabu gani ambayo watapewa wale ambao hawatakuwa wamerasmisha ndoa zao kufikia mwisho wa mwaka huu.

source:muungwana

0 comments:

Post a Comment