Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na kusababisha mauaji ya raia na polisi.
Akizungumza kwa mara ya kwanza, mbele ya vyombo vya habari, baada ya kuteuliwa katika nafasi hiyo, siku chache zilizopita, Mkuu wa Jeshi la polisi Simon Sirro amesema changamoto iliyopo kwa sasa ni tatizo la mkoa wa Pwani ambako raia wema wamekuwa wakiuawa.
Katika kukabiliana na hali hiyo amesema wanaendelea na operesheni mbalimbali kuhakikisha kwamba vitendo hivyo haviendelei na wanaojihusisha na mauaji wakikamatwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
''..Suala la Ikwiriri suala la Rufiji ni suala la muda mfupi...'' Alisema Sirro
Amesisitiza kuwa wahalifu ni kikundi cha watu wachache na kijue kuwa wao ni Watanzania, hivyo haoni sababu waendelee kuwafanyia wenzao ubaya.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza kutoa takriban dola elfu 5, ama shilingi milioni 10, kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazofanikishwa kukamatwa kwa wahalifu wa mauaji ya wananchi na polisi mkoani Pwani.
Katika siku za hivi karibuni Tanzania imeshuhudia mauaji yanayofanywa na watu wasio julikana katika wilaya za Rufiji, Mkuranga na Kibiti mkoani Pwani, hali ambayo imeleta wasiwasi kwa raia.
source:bbc