CHAMA cha ACT-Wazalendo kimelaumu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama kufuatia kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kutawanya maandamano ya watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam juzi.
Chama hicho pia kimemtaka Waziri Mwigulu kuiomba radhi jumuiya ya watu wenye ulemavu kutokana na kitendo hicho.
Aidha, ACT imemtaka Waziri Mhagama kuhakikisha madai ya watu wenye ulemavu yanasikilizwa na kutolewa majibu.
Polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu wenye ulemavu waliokuwa wamefunga Barabara ya Sokoine jijini Dar es Salaam Ijumaa, kabla ya kukamata 40 kati yao, akiwamo mwanamke mmoja.
Walemavu hao walikuwa na lengo la kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuwasilisha malalamiko ya bajaj zao kukamatwa kamatwa na askari wa usalama barabarani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu tukio hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema wanalaani vikali Jeshi la Polisi kutumia nguvu "kubwa" kwa watu wenye ulemavu ambao hawakuwa na silaha yoyote.
"Tunamtaka Waziri mwenye dhamana ya Jeshi la Polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuiomba radhi jumuiya ya watu wenye ulemavu hapa nchini kwa kitendo cha Jeshi la Polisi na kuhakikisha vitendo kama hivi havirudiwi tena," alisema Shaibu.
Shaibu alisema Waziri Mhagama naye anapaswa kuhakikisha madai ya walemavu yanasikilizwa.
Pia ACT iliitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuchukua hatua kali kwa jeshi hilo kufuatia vitendo vilivyofanywa na askari wake dhidi ya walemavu.
Alisema madai ya watu wenye ulemavu yanalindwa na mikataba ya kimataifa pamoja na sheria za nchi, ikiwamo ibara ya tisa ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye ulemavu ya mwaka 2006.
Alisema ibara hiyo inatoa haki kwa watu wenye ulemavu kuondolewa vikwazo vya kimiundombinu vinavyozuia uwezo wao wa kwenda watakako.
Alisema hata ibara ya 15 ya mikataba husika inazuia mateso na adhabu zinazokwenda kinyume na utu wa watu wenye ulemavu.
WATU 40"Tunaamini kwa dhati kuwa Jeshi la Polisi lingeweza kuwakamata na kuwazuia watu hao wenye ulemavu ambao hawakuwa na silaha yoyote, bila kutumia nguvu kubwa kama walivyofanya," alisema Shaibu.
"Jeshi la Polisi lilipaswa kuwaongoza walemavu hao hadi Manispaa ya Ilala kwenda kuwasilisha kilio chao."Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni aliliambia Nipashe mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa askari wake walilazimika kutumia mabomu kama njia ya kuwakamata watu hao.
Kamanda Hamduni alisema kutokana na kitendo hicho, polisi ilikuwa ikiwashikilia watu 40 akiwamo mwanamke mmoja.
Kamanda Hamduni alisema baada ya polisi kufika eneo hilo na kutoa amri mara tatu ya kuwataka kutawanyika, walemavu walikaidi.
Alisela ukaidi huo uliwaacha polisi wakiwa hawana njia nyingine zaidi ya kutumia mabomu ya machozi.Alisema nguvu hiyo ya kutumia mabomu ilikuwa na lengo la kurahisisha ukamataji wa watu hao waliokaidi amri ya polisi kutawanyika