Saturday, 10 June 2017

Afc Leopards uso kwa uso na Gor Mahia kwenye fainali ya Sportpesa Super Cup

Washindi wa nusu fainali za SportPesa Super Cup zilizofanyika Juni 08, 2017 Jijini Dar es Salaam, wanatarajiwa kukutana uso kwa uso kwenye mechi ya fainali ya kuwania kombe la michuano ya SportPesa Super Cup siku ya Jumapili ya tarehe 11, Juni 2017 itakayochezwa kwenye dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam.

Katika mechi za nusu fainali, AFC Leopards walipambana na mabingwa wa Ligi kuu Tanzania bara, Klabu ya Yanga na kuwang’oa kwa mikwaju ya penati 4-2 huku Gor Mahia kwa upande wao wakiifungasha virago timu ya Nakuru All Stars FC kufuatia ushindi wa magoli 2-0 ambayo yalitiwa kimiani na mshambuliaji Medie Kagere na George Odhiambo.    

Timu za Yanga na Nakuru All Stars FC ambazo ziling’olewa kwenye hatua ya nusu fainali, zilikabidhiwa medali za shaba na kiasi cha dola za kimarekani 5000 wakati wenzao (Gor Mahia na AFC Leopards) ambao wamefuzu kucheza fainali wakiwania kiasi cha dola za kimarekani 30,000.

Akizungumzia mshindano ya SportPesa Super Cup kwa ujumla, Mkurungezi wa Utawala na Utekelezaji SportPesa Tanzania Ndugu Abbas Tarimba alisema; “Michuano ilikuwa migumu ingawa timu zetu za Tanzania zimeaga katika hatua za awali lakini ni nafasi nzuri kwetu kama Tanzania kujipanga vizuri zaidi ili kuboresha sekta ya michezo na kufanya timu zetu kushika nafasi za juu maana kwa sasa tumeweza kutambua changamoto mbalimbali na jinsi ya kuzikabili.

SportPesa ni kampuni nguli ya michezo ya kubashiri inayojulikana kimataifa yenye makao yake makuu nchini Kenya ambayo imeanza rasmi shughuli zake nchini Tanzania Mei 9 mwaka huu na mpaka sasa imeshaingia makubaliano rasmi ya udhamini na vilabu vya Simba, Yanga na Singida United ikiwa imejidhatiti katika kuinua ba kuendeleza sekta ya michezo nchini.


source:muungwana

0 comments:

Post a Comment