Monday, 19 June 2017

Hoja 6 moto mkali kwa serikali bungeni

MJADALA wa mapendekezo ya makadirio ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 unatarajiwa kuhitimishwa leo mjini hapa huku hoja sita zikionekana kuwa mtihani mgumu kwa serikali kuzitolea majibu kesho wakati inahitimisha mjadala huo kabla ya wabunge kupiga kura ya wazi ya kuipitisha kesho 

Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano wa Bunge la Bajeti, baada ya mjadala wa bajeti ya serikali kuhitimishwa leo na wabunge kupitisha bajeti kwa kura ya wazi kesho, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, atawasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi.

Kwa siku ya nane mfululizo wabunge wamekuwa wakijadili mapendekezo ya makadirio ya bajeti hiyo ya Sh. trilioni 31.7 huku mjadala huo ukionekana 'kutekwa' na sakata la makinikia.

HOJA SITA MOTOUtunishaji wa mfuko wa maji, mfuko wa mazingira, ujenzi wa reli ya kisasa Dar es Salaam -Tanga-Musoma  na ujenzi wa zahati kila kijiji na kituo cha afya kila kata ni miongoni mwa hoja sita ambazo zinatarajiwa kuwa mtihani mgumu kwa serikali wakati wa kuhitimisha mjadala huo kesho.

Nyingine ni uimarishaji wa Kampuni ya Simu (TTCL) na kufutwa kwa ada ya mwaka ya leseni za magari yaani 'road licence fee'.  

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia, aliliambia Bunge Jumatatu iliyopita kuwa kamati yake ilipokea hoja zilizojitokeza wakati wa kujadili na utekelezaji wa bajeti za wizara mbalimbali kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 na makadirio ya bajeti zake kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuliibuka hoja ya TTCL iongezewe mtaji ili iweze kuchangia pato la taifa.

Alisema kamati yake ilikubaliana na hoja hiyo na kupendekeza kwa kuanzia kampuni hiyo ipewe Sh. bilioni 295.2 kama mtaji, lakini majibu ya serikali hayaonyeshi ni kiasi gani itaipatia TTCL.

Ghasia alisema hoja ya pili ilihusu kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam-Musoma kupitia Tanga, Moshi na Arusha na kwamba kamati ilipendekeza fedha za mfuko wa reli zitumike kulipia gharama za upembuzi yakinifu na upembuzi wa kina.

Hoja ya tatu ilitoka Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo inataka Mfuko wa Mazingira uwezeshwa kifedha na ilipendekeza ikatwe asilimia tano kutoka kwenye vyanzo 11 vinavyohusu tozo mbalimbali za wizara na taasisi ili mfuko huo upate fedha za kujiendesha.

Ghasia alisema kuwa katika majibu yake mbele ya kamati hiyo, serikali haikuonyesha kuwa kiasi cha Sh. bilioni 13 kinaweza kupatiana kutoka vyanzo husika.

Hoja ya nne ni kuongeza bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kuongeza tozo ya Sh. 50 kwa kila lita ya petroli na dizeli kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Maji.

Ghasia alisema kamati yake inapendekeza asilimia 70 ya makusanyo itumike kwa ajili ya kuboresha maji vijijini na asilimia 30 ya makusanyo itumike kwa ajili ya maji maeneo ya mijini.

Alisema hoja ya tano ilitoka kwenye Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambapo kamati yake ilitaka kujua gharama halisi za ujenzi wa kila kituo cha afya na zahanati pamoja na kiasi cha fedha ambacho kimetengwa na serikali na kutekeleza ujenzi huo katika mwaka ujao wa fedha.

Alisema majibu ya serikali ni kuwa imetenga Sh. bilioni 69 kwa ajili ya kuanza na kukamilisha ujenzi wa maboma ya zahanati 1,538 na vituo vya afya 244 na kwamba baada ya mashauriano na serikali, kamati yake ilikubali majibu hayo.

Hoja hiyo ililazimika kufikishwa mbele ya kamati hiyo baada ya wabunge wote kuungana kuitaka serikali itekeleze ahadi yake ya kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata ili kupunguza vifo vya uzazi ambavyo kwa sasa ni 556 katika kila vizazi hai 100,000 nchini.

Kuhusu kufutwa kwa ada ya mwaka ya leseni za magari yaani, Ghasia alisema imeondoa kero kubwa kwa wananchi hivyo kurudisha imani kwa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Alisema hatua hiyo pia itaongeza mapato ya serikali kuliko ilivyokuwa awali na kwamba kamati inashauri kutumia kiasi cha Sh. 40 kitakachoongezwa kwenye mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kipelekwe kwenye mfuko wa maji kwa ajili ya miradi ya maji vijijini.

Mbali na hoja hizo zilizofikishwa mbele ya kamati ya Ghasia, wabunge wa upinzani wakati wa mjadala wamekuwa wakilalamikia kitendo cha serikali kuu kuchukua baadhi ya kodi za serikali za mitaa zikiwamo za majengo, ardhi na mabango ya matangazo.

0 comments:

Post a Comment