Tuesday, 13 June 2017

Hawa wote motoni

KIMENUKA! RAIS John Magufuli ameagiza kukamatwa na kuhojiwa kwa waliokuwa mawaziri, kamishina wa madini, wanasheria wakuu (AG) na waliokuwa watumishi katika idara mbalimbali za serikali zilizoruhusu usafirishaji wa madini na kuikosesha serikali mapato ya matrilioni ya fedha tangu mwaka 1998.

Rais Magufuli ambaye alionekana akizungumza kwa uchungu mwingi jana baada ya kupokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa mchanga wa madini (makinikia) kuangalia masuala ya kiuchumi, kisheria na mikataba ya madini iliyoingiwa na Tanzania kwa kampuni ya Acacia, alitoa amri hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Prof. Nehemia Osoro, ilitaja vyeo na majina ya viongozi waliohusika kuliingiza taifa kwenye hasara ya mabilioni ya fedha, ikiwamo kuruhusu wawekezaji hao kutolipa fedha yoyote serikalini.

Kamati hiyo iliundwa na Rais Magufuli Aprili 10 mwaka huu, ikiwa na wajumbe nane wenye taaluma za sheria na uchumi, pia ilifichua kuwa kampuni ya migodi ya Acacia inafanya kazi zake nchini kinyemela baada ya kutosajiliwa na mamlaka yenye wajibu huo.

UCHUNGUZI MAWAZIRI, AG WASTAAFU
Kamati hiyo ambayo ilikiri kukumbana na changamoto nyingi wakati wa utekelezaji wa majukumu yake ikiwamo kutaka kuhongwa na kutishiwa maisha, ilitoa mapendekezo 21 yaliyoridhiwa yote na Rais Magufuli kwa asilimia 100.

Aidha, kamati ilitoa mapendekezo 21 ambayo rais aliyapokea na kutaka yafanyiwe utekelezaji kwa asilimia 100, ikiwamo kumwagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Palamagamba Kabudi, kuunda timu ya wanasheria kupeleka muswada wa marekebisho ya sheria hiyo.

Ripoti hiyo ilipokewa ikiwa ni siku 19 tangu Rais alipopokea ripoti nyingine ya kuchunguza kiwango, ubora na aina ya madini yaliyokuwapo kwenye mchanga huo kutoka kwa wataalamu wa madini, miamba na kemia.

Waliotajwa katika ripoti iliyowasilishwa jana na hivyo kutakiwa wachunguzwe ni waliowahi kuwa mawaziri katika serikali za awamu ya tatu, nne na tano ambao ni Nazir Karamagi, marehemu Dk. Abdallah Kigoda, Daniel Yona, William Ngeleja na Prof. Sospeter Muhongo.

Wengine ni waliowahi kuwa wanasheria wakuu wa serikali Andrew Chenge (sasa Mwenyekiti wa Bunge) na Johnson Mwanyika; wengine ni Felix Mrema, Maria Ndosi, aliyekuwa Kamishina wa madini nchini, Dk. Dalali Kafumu na pia Paulo Masanja na Ally Samaje.

Mara baada ya Rais Magufuli kueleza kwa uchungu jinsi Tanzania ilivyoibiwa kwa muda mrefu, alisema baada ya kuridhia mapendekezo hayo viongozi wote waliohusika kwa namna yoyote wachunguzwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, Rais alieleza masikitiko yake kwa viongozi wa wizara husika kuridhika na taarifa za mezani bila kufika kwenye maeneo ambako mchanga huo unapelekwa huku akiwataja mawaziri na makatibu wakuu waliowahi kusafiri kwenda Ulaya na wengine waliosaini mikataba ya uchimbaji wakiwa hotelini.

“Mungu alitupa raslimali nyingi ili ziwanufaishe Watanzania. Ni eneo ambapo kila kitu kipo. Madini tuliyonayo ni ya kila aina na siyo machache.

Tuna dhahabu, copper, silver, berlium…Tanzania tumepewa gesi … na Helium ambayo inapatikana katika nchi tatu tu dunia na Tanzanite inayopatikana Tanzania tu,” alisema na kuongeza: 

“Lakini pamoja na mali yote hii Mungu kutupendelea, Watanzani tumeendelea kuwa maskini. Nina uhakika hata shetani aliko huko anatucheka kuwa umaskini wetu ni wa kujitakia.

Lakini inawezekana shetani huyo huyo aliwatumia baadhi ya Watanzania, wengine wakiwa viongozi, kuifanya Tanzania kuwa maskini. Lakini bado anawatumia baadhi ya viongozi wengine kupinga juhudi hizo.”

Alisema wapo Watanzania wana maisha ya ajabu kwa kuwa kuna watoto wanakufa kwa kukosa dawa, wapo wanaolazwa hospitali na kutoka katika hali wasiyostahilina, wapo wakulima wanaokosa pembejeo kwa ajili ya mazao, huku nchi ikikopa kwa ajili ya kujenga miundombinu na wao wakikosa maji na kufa kwa kipindupindu huku mali zao zikiendelea kusombwa.

Alisema Watanzania zaidi ya 1,000 walifariki kwa ajali ya MV Bukoba lakini serikali imeshindwa kupeleka miundombinu kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

“Lakini wapo Watanzania wenzetu waliopewa madaraka na Watanzania kwa ajili ya kusimamia raslimali zetu wamekuwa sehemu ya watu wa kuwaibia Watanzania maskini,” alisema Magufuli.

CHENGE KIMYA
Mwenyekiti wa Bunge, Chenge, ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa takribani miaka 12, alikataa kuzungumzia yaliojiri kwenye ripoti iliyosomwa Ikulu jana.

“Sizungumzi chochote,” hilo ndilo lilikuwa jibu la Chenge alipofuatwa na waandishi wa habari waliotaka kupata maoni yake kuhusiana na suala hilo jana.

NGELEJA ANENA
Waziri wa zamani  wa Wizara ya Nishati na Madini, Ngeleja, yeye alisifu hatua iliyochukuliwa na Rais Magufuli na kuwataka Watanzania wamuunge mkono.
Alisema ni kweli Tanzania imekuwa ikinyonywa kwa muda mrefu kwenye sekta ya madini kwa sababu ilistahili kupata zaidi ya kile inachopata sasa.

 “Nimesikiliza ripoti iliyowasilishwa na nimemsikiliza Rais alivyokuwa anazungumza kwa hisia za kizalendo… nadhani kuna haja kwa Watanzania wote kumuunga mkono kwenye kazi hii ngumu,” alisema Ngeleja na kuongeza:

 “Ukiangalia tumefikaje hapa ni hii Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Kama tungekuwa makini katika kuitekeleza tusingefika hapa. Kuna vitu vilikosewa.”

Hata hivyo, Ngeleja alikataa kuzungumza chochote kuhusu watuhumiwa waliotajwa kwenye ripoti hiyo kuwa wanastahili kuchukuliwa hatua, wakiwamo mawaziri wa zamani.

Ngeleja aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, kwenye serikali ya awamu ya nne, kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2012 alipojiuzulu.

Wengine waliotajwa katika ripoti hiyo hawkaupatikana jana ili kutoa maoni yao.

Mbunge wa Vunjo, (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alisema ushabiki wa kisiasa ndio umeifikisha nchi pabaya kwa sababu sheria nyingi hupitishwa bungeni kwa ushabiki wa vyama badala ya kuangalia maslahi ya taifa.

“Hizi Sheria wakati zinapitishwa miaka ishirini iliyopita mimi nilikuwa humu bungeni. Niliona tulivyozipitisha kwa ushabiki. Sasa matokeo yake ndiyo haya. Ndiyo maana nashauri tuwe tunaweka uzalendo mbele badala ya vyama,” alisema Mbatia.


ACACIA HAIPO KISHERIA
Katika mapendekezo 21 yaliyowasilishwa na kamati na kisha Rais Magufuli kuyaridhia yote, ni pamoja na Serikali, kupitia Msajili wa Makampuni, ichukue hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya Acacia Mining Plc ambayo imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini kinyume cha matakwa ya Sheria. 


Related Posts:

0 comments:

Post a Comment