Saturday 17 June 2017

Hizi ndizo adhabu za watuhumiwa wa Makinikia wakikutwa na hatia

BAADHI ya wanasheria, wabunge waliomo katika kamati inayoshughulikia sheria na katiba na pia wachambuzi wa masuala ya kisheria, walisema kuwa yeyote miongoni mwa wanaochunguzwa sasa na vyombo vya dola anaweza kukumbana na adhabu ya kifungo cha miaka mingi jela au kufilisiwa mali zote alizozipata kwa njia haramu ikiwa mahakama itamkuta na hatia, hasa kutokana na kosa la uhujumu uchumi.

Ilielezwa kuwa miongoni mwa mali ambazo zinaweza kufilisiwa kwa wale watakaothibitika mahakamani kuwa wana hatia ya uhujumu uchumi ni pamoja na nyumba, mashamba, magari, fedha kwenye akaunti zao benki na mali nyinginezo kulingana na vile itakavyoamuliwa na mahakama.

“Kati ya makosa mazito mahakamani ni pamoja na la uhujumu uchumi…anayekutwa na hatia katika kosa hilo hukumbwa na adhabu kali ikiwamo hiyo ya kufilisiwa na pia kuna kufungwa miaka mingi gerezani,” alisema mmoja wa wachambuzi wa masuala ya sheria.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba, alisema upo uwezekano kwa watakaokutwa na hatia kukumbana na adhabu nzito mahakamani pindi wakikutwa na hatia.

Hata hivyo, alitahadharisha kuwa wale wote wanaotajwa sasa ni watuhumiwa tu na kwamba, iwapo watabainika wana jinai na rushwa, ndipo majalada yao yatapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kisha kufikishwa mahakamani.

“Uchunguzi utakaowabaini na DPP kuridhika na mashtaka kwamba kuna rushwa ndani yake ndipo jalada hupelekwa mahakamani,” alisema Kibamba.
Alisema kama mhusika anakutwa na kosa la uhujumu uchumi, mwenye kuamua adhabu yake huwa ni mahakama.

“Mwamuzi ni mahakama pekee ambayo inaweza kuamua kwamba mtuhumiwa wa uhujumu uchumi ahukumiwaje… lakini ikibainika kuna hatia, mtu anaweza kufungwa kifungo cha miaka 30, kwa nchi kama Brazili au Venezuela hapo uhujumu uchumi tunasema ni miaka hadi 50 au 60,” alisema Kibamba.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadam (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema iwapo watuhumiwa wakibainika walifanya makosa ya kiofisi na ikiwamo waziri kushindwa kusimamia au kuwajibika katika majukumu yake, itakuwa ni makosa ya kiutawala ambayo kwa hivi sasa hayatawahusu waliokuwa nje ya ofisi.

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema kutokana na kosa hilo linalowakabili watuhumiwa kuwa kubwa, wakibainika kisheria walihusika kwa namna moja au nyingine wanaweza kuhukumiwa kifungo, ama faini pamoja na mali zao kufilisiwa kulingana na sheria ya jinai ya kiuchumi.

Alisema kosa la jinai lina adhabu tofauti, ikiwamo kifungo au faini na kila kosa lina adhabu zake, ikiwa ni pamoja na kuhudumia jamii kwa kufanya usafi maeneo mbalimbali ya umma au kuripoti mahakamani kila siku.

“Mali inaweza ikarudi kwa umma kwa kuwa si za kwao. Iwapo wakibainika wana hatia, kisheria adhabu inaweza kuwa pamoja na kufilisiwa,” alisema.

Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, alisema adhabu ya watu waliotajwa kwenye sakata la mchanga wa madini na kuthibitika kuwa wana hatia itategemeana na vifungu watakavyoshitakiwa navyo, lakini mojawapo ya maamuzi inaweza kuwa ni kufilisiwa mali zao.

Hata hivyo, alisema siyo sahihi kuamini moja kwa moja kuwa kila mmoja atashtakiwa kwa sababu hilo linategemea namna atakavyojieleza.

“Kwa hiyo si lazima mtu afunguliwe mashtaka. Inategemea yeye atakavyojieleza na wakaangalia wakaona kuna kosa,” alisema Mchengerwa.

Alisema kama kuna jambo lilifanywa nje ya sheria kwa ajili ya mtu kujinufaisha yeye mwenyewe, sheria itaangalia ukubwa wa mchango wake katika hasara iliyopatikana halafu ndipo itaangaliwa kama kuna kosa.

“Huwezi mfungulia mashtaka mtu kama huna ‘element’ ya kosa. Kwa mfano, unaweza kusema mtu ameingia mkataba ameisababishia hasara nchi… lakini ameingia mkataba kwa mujibu wa sheria,” alisema na kuongeza kuwa ni lazima kuwapo na viashiria vya kosa ndipo mtu atashtakiwa kwa kosa la jinai.

Aidha, Mchengerwa ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema katika sakata la makinikia kuna uwezekano mtu akashtakiwa kuwa kwa kosa la kuhujumu uchumi kama alifanya makosa nje ya sheria inavyomtaka na kusababisha hasara.

Alisema kuhujumu uchumi kuna makosa mengi na miongoni mwa adhabu zake ni mhusika kutakiwa alipe mara mbili au mara tatu ya fedha inayotakiwa au kifungo cha miaka 5 au 10.

“Masuala ya uhujumu uchumi mara nyingi huangalia hasara uliyosababisha na kama hiyo fedha hakuna mwisho wa siku mahakama inaweza kuamua,” alisema.

Ripoti iliyowasilishwa na Prof. Osoro ilionyesha baadhi ya viongozi waliokuwa katika awamu mbalimbali za uongozi, walishiriki kulikosesha taifa mapato kutokana na maamuzi yao mbalimbali. Ilielezwa zaidi kuwa nchi inaweza kuwa imepoteza Sh. trilioni 489 katika kodi na mali (madini) tangu mwaka 1998 na kati ya fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa Sh. trilioni 108.

0 comments:

Post a Comment