Monday, 19 June 2017

Simba yatumia Mil. 100/ kumshawishi Niyonzima

NI UMAFIA TU! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima kudaiwa kujiunga na Klabu ya Simba kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kupewa ofa ya Sh. milioni 100.

Habari zilizopatikana jana jioni zinasema Niyonzima amekubali kujiunga na Simba baada ya viongozi wa klabu hiyo kumpa fedha hizo za usajili.

Kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Bara, Niyonzima ambaye amebakisha mwezi mmoja kwenye mkataba wake na Yanga, alikuwa akihusishwa kutaka kujiunga na Simba.

Taarifa zinadai kuwa Simba waliongea na Niyonzima kabla hajaenda Rwanda kujiunga na timu yake ya Taifa, lakini akataka viongozi hao kuwasiliana na wakala wake ambapo Simba walifanya hivyo na kupewa dau walilokuwa wakilitaka.

Aidha, Yanga iliwasiliana na Niyonzima akiwa Rwanda baada ya kusikia Simba wamewasiliana naye na hivyo wakamuahidi ofa nono ili asisajiliwe na Simba.

Baada ya kusikia Yanga wamewasiliana na Niyonzima, Simba walimtuma mtu kwenda Rwanda kufanya mazungumzo na mchezaji huyo, lakini wakala wake aliwataka wamsubiri Niyonzima Dar es Salaam kwa kuwa alikuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa.

Niyonzima alipowasili nchini juzi usiku alipokelewa na kigogo mmoja wa Simba huku Yanga wakiwa hawafahamu kama nyota huyo ametua nchini.

Imeelezwa Yanga walimuandalia nyota huyo dau la Sh. milioni 60 ili asaini mkataba wa miaka miwili, lakini tajiri mmoja wa Simba alimuhakikishia kumpa dau la Sh. milioni 100.

Kabla ya kupewa dau hilo, Yanga waliongezea dau lao na kufikia Sh. milioni 80 ambazo hata hivyo, hazikumshawishi nahodha huyo wa Rwanda kusaini nao mkataba mpya.

Aidha, pia Simba juzi ilimalizana na kiungo na nahodha wake, Jonas Mkude kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili.

Mkude pia alikuwa akiwindwa na Yanga iliyoibomoa Simba kwa kumsajili mshambuliaji wao, Ibrahimu Ajib.

0 comments:

Post a Comment