Tuesday 13 June 2017

Wananchi watema cheche, wataka Marais wastaafu wachunguzwe

Mikoani. Wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wamemshauri Rais John Magufuli kufanya mabadiliko ya Katiba na kuhakikisha diplomasia ya uchumi haivurugiki kutokana na sakata la mchanga wa madini (makinikia).

Wakitoa maoni yao jana, baadhi ya wananchi walisema licha ya viongozi walioongoza Wizara ya Nishati na Madini, wanasheria wakuu na watendaji wengine wa Serikali kutajwa katika ripoti ya kamati ya pili ya uchunguzi wa makinikia, Katiba ibadilishwe ili iweze kuruhusu marais wastaafu kuchunguzwa na kushtakiwa.

Maoni kutoka Kanda ya Ziwa

Baadhi ya wananchi kutoka mikoa ya Mara, Geita, Shinyanga, Mwanza na Kagera pia walipendekeza utaratibu wa kisheria ufanyike kutaifisha mali za watu binafsi na kampuni zilizohusika na hujuma katika sekta ya madini.

Mkazi wa mjini Tarime, Abdul Ahmed, alishauri kampuni zilizobainika kufanya udanganyifu zifilisiwe na watendaji wake kushtakiwa au kufukuzwa nchini. Pia alipendekeza Katiba na sheria zibadilishwe kutoa fursa ya uchunguzi wa kijinai dhidi ya marais wastaafu kubaini iwapo walihusika au walijua na kunyamazia hujuma katika sekta ya madini.

“Nadhani tubadilishe hili ili kuongeza nidhamu na hofu kwa wanaokabidhiwa dhamana ya uongozi,” alisema Ahmed.

Alisema uwapo wa kifungu cha viongozi wote kuwajibishwa kwa makosa ya jinai wanayotenda au kunyamazia kwa nafasi zao, kitarejesha nidhamu ya utumishi.

Wasemavyo Manyara, Arusha

Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Manyara (Marema) na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Arusha (Angonet), wameunga mkono hatua ya Rais lakini wakamtaka kukutana na mabalozi wa nchi zinakotoka kampuni zinazochimba madini ili kuzungumzia yaliyobainishwa na kamati za uchunguzi.

Kwa nyakati tofauti wenyeviti wa Marema, Sakidi Mnenei na wa Angonet, Petro Ahham walisema Rais ana nia njema katika sakata la utoroshwaji madini lakini ili kuungwa mkono zaidi, wadau wengine wanapaswa kuhusishwa.

Mnenei alisema ili kuepuka kuvuruga diplomasia ya kiuchumi ni vyema sasa Rais Magufuli akakutana na mabalozi wa nchi ambazo kampuni hizo zinatoka ili kuwapa taarifa na mapendekezo ya Serikali hasa baada ya kubainika kuwapo wizi.

“Nia ya Rais ni nzuri tumeibiwa kiasi cha kutosha sasa, tutoke hapa bila kusababisha athari nyingine za kiuchumi na ni vyema mikataba ya madini ipelekwe bungeni na ipitiwe upya,” alisema.

Ahham alisema vita ambayo Rais anapigana ni kubwa lakini anapaswa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) na asasi zingine ili kusaidia ushindi.

Mkurugenzi wa Shirika la Haki Madini, Aman Mustapha licha ya kueleza kuwa anaunga mkono jitihada za Serikali, alisema upotevu wa fedha ambao unatajwa unaonyesha udhaifu mkubwa serikalini.

Ushauri kutoka Mbeya

“Tunamshukuru Rais kwa uzalendo lakini asiwaonee huruma, achukue uamuzi wa kuzuia mali zao ndipo hatua ya kuwapeleka mahakamani ifuatwe,” alisema Aggrey Kandonga ambaye ni muasisi wa Chadema mkoani Mbeya.

Diwani mstaafu wa Kata ya Itezi jijini Mbeya, Frank Maemba alisema watumishi wa BoT wanapaswa kuwajibishwa kwa kuwa wao ndio wanaosimamia uchumi wa nchi.

Source: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment