WABUNGE watatu, wakiwamo Andrew Chenge na William Ngeleja ambao Kamati ya pili ya Rais kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na makinikia Jumatatu iliyopita ilishauri wachunguzwe, jana walitoa mchango kwa kanisa.
Wakati Chenge ni Mbunge wa Bariadi, Ngeleja anawakilisha wananchi wa jimbo la Sengerema.
Kamati ya Profesa Nehemia Osoro iliyokuwa imeundwa na wataalamu wa uchumi, sheria na takwimu iligundua nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka Sh. trilioni 500 katika kodi na mali kutokana na udanganyifu ama udhaifu wa utendaji wa wadau katika biashara ya makinikia, tangu mwaka 1998 mpaka sasa.
Maofisa wa serikali waliokosolewa na kupendekezwa kuchunguzwa ni pamoja na mawaziri wa madini, wanasheria wakuu wa serikali na makamishna wa madini, wote waliopita.
Mbunge mwingine aliye kwenye kibano cha kamati ya Prof. Osoro na akatoa mchango wa fedha katika harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa jengo la kisasa la Baraza la Kikristo (CCT) mjini Dodoma jana ni Dk. Dalaly Kafumu (Igunga).
Akizungumza katika hafla hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema anachangia Sh. milioni 10, lakini pia angewasilisha michango ya wabunge wengine ambao hawakufika akiwamo Chenge na Dk. Kafumu ambao kila mmoja alitoa Sh. 500,000.
"Mimi nachangia shilingi milioni kumi, lakini ninayo michango ya wabunge ambao hawakufika leo hii katika harambee hii akiwamo mheshimiwa Chenge ambaye anatoa Sh. 500,000," alisema Ndugai."Mheshimiwa Dk. Kafumu naye (anatoa) Sh. 500,000."
Wakati wabunge wengine waliohudhuria harambee hiyo walipoanza kuchangia, Goodluck Mlinga wa Ulanga aliahidi kutoa Sh. milioni 1.5 na kusema pia ametumwa na Ngeleja kuwasilisha ahadi yake.
Mlinga alisema Ngeleja ambaye alimwambia kiasi ambacho atakachotoa yeye mahali hapo, Waziri wa Nishati na Madini huyo wa zamani angetoa mara mbili yake.
"(Hivyo) mimi natoa shilingi milioni moja na nusu," alisema na kumaanisha Ngeleja atachangia Sh. milioni tatu.Wakati Kafumu anaingia kwenye mapendekezo ya kamati ya Prof. Osoro kwa kuwa kamishna wa madini wa zamani, Chenge alikuwa mwanasheria mkuu (AG).
Awali katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Mchungaji Moses Matonya alisema ujenzi wa jengo hilo unakadiriwa kutumia zaidi ya Sh. bilioni tatu na litakuwa la ghorofa 10.
"Tunahitaji kiasi cha Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanzia hatua za wali za ujenzi, hasa katika michoro," alisema na "harambee hii itaendelea katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kufanikisha jengo hili ambalo litakuwa la kisasa zaidi kuendana na makao makuu."
source:muungwana
0 comments:
Post a Comment