Wednesday, 14 June 2017
Home »
» Hili ndilo janga la tatu alilolipata Mbowe
Hili ndilo janga la tatu alilolipata Mbowe
Masaibu yanazidi kumkumba Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe baada ya Serikali kung’oa miundombinu ya umwagiliaji katika shamba lake.
Hilo ni janga jingine kwa Mbowe baada ya miezi michache iliyopita kutajwa katika sakata la dawa za kulevya na kubomolewa kwa ukumbi wake maarufu wa Bilicanas.
Mbali ya kung’oa miundombinu hiyo, Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (Nemc), imemtoza faini ya Sh18 milioni kwa kuendesha kilimo ndani ya mita 60 kutoka chanzo cha maji.
Mbowe amezungumzia tukio hilo na kusema utaratibu mzima ulikuwa ni batili na ni matumizi mabaya ya madaraka.
“Ni bahati mbaya sana tunaruhusu nchi kuendeshwa kwa hila na husda kujaribu kuzima sauti za watu kushauri Taifa letu. Taarifa hiyo nimeipata na mimi kwa sasa niko Dodoma,” Mbowe alisema jana, “Agizo na utaratibu mzima uliotumika ni batili. Tulipopata agizo la Nemc tuliwajibu kuwa sheria inaruhusu kukata rufaa na tulikata rufaa kwa waziri mwenye dhamana na tunasubiri majibu.”
Alisema hatua hiyo imechukuliwa wakati akisubiri rufaa hiyo kwa waziri na kwamba sasa anawasiliana na wanasheria wake ili kujua hatua za kuchukua.
Kazi ya kung’oa miundombinu ya shamba hilo la kampuni ya Kilimanjaro Veggies linalomilikiwa na Mbowe ilifanyika chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa na maofisa wa Nemc.
Shamba hilo la kilimo cha kisasa cha banda kitalu (green house), lililopo katika Kijiji cha Nshara Mashame, linadaiwa kuwa ndani ya mita 60 kutoka Mto Weruweru, kinyume cha sheria.
Akizungumza katika eneo la tukio, Byakanwa alisema Januari 20 alifika katika shamba hilo la mbogamboga na kuamuru kusitishwa kwa shughuli zote za kilimo.
Alisema baada ya kusitisha shughuli hizo, Januari 23 akiwa ameambatana na wanasheria wake, Mbowe alimfuata ofsini na kufanya kikao pamoja na maofisa wa Nemc na Bonde la Pangani (PWB).
“Katika kikao kile tulimweleza kuwa shughuli anazozifanya ziko kinyume cha sheria. Baada ya maelezo, yeye mwenyewe akasema amewekeza hela nyingi sana na alitaka kuwafundisha vijana,” alisema.
Alisema katika kikao hicho, Mbowe aliomba apewe muda wa miaka miwili awe amevuna na kuondoa, lakini alikataliwa ombi hilo na kupewa miezi minne.
“Nilimwagiza ndani ya muda huo awe amevuna na kuondoa mazao yote pamoja na miundombinu yote na asiwe ameanzisha kilimo kipya. Lakini leo (jana) tumekuja kuna kilimo kipya kimeanzishwa,” alisema.
Byakanwa alisema katika mazungumzo ya Januari, aliwataka pia Nemc kufanya utafiti wa uharibifu wa mazingira na kubainisha kwamba tathmini hiyo imeonyesha kuwapo kwa uchafuzi wa maji ya Mto Weruweru.
“Miezi minne niliyokubaliana naye (Mbowe) ilikuwa inaanza Januari 23 hadi Mei 25. Leo tunapoongea ni Juni 13 maana yake zimepita siku 20 zaidi...”
Mkuu huyo wa wilaya alisema hataki kuwa sehemu ya ushuhuda wa watu waliokaa kimya wakishuhudia uharibifu huo wa mazingira kwa kuwa tu anayelima katika chanzo hicho ni Mbowe.
“Sheria ninayoisimamia sio ya halmashauri wala ya DC, ni sheria ya Bunge. Sisi sote ni mashuhuda wa madhara ya uharibifu wa mazingira,” alisema na kuongeza:
“Kwa vile kilimo hiki kinakinzana na Sheria ya Mazingira, watu wa Nemc wameshatoa adhabu. Huyu bwana anatakiwa kulipa Sh18 milioni zinazotokana na uharibifu wa mazingira.”
Mkuu huyo wa wilaya alisema Serikali imeamua kuondoa miundombinu yote shambani hapo na Mbowe atawajibika kulipa gharama zilizoingiwa katika kazi hiyo.
“Naomba nieleweke kwa wananchi wote kuwa hili hatulifanyi kwa kumuonea mtu, bali kusimamia sheria. Wapo watu wanaweza kugeuza hili suala kuwa la kisiasa. Sikumtuma Mbowe,” alisisitiza.
Mkaguzi wa Mazingira wa Nemc, Novatus Mushi alisema Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, inamtaka kila anayeanzisha mradi, afanye tathmini ya athari ya mazingira.
“Alipoanzisha (Mbowe) huu mradi hakufanya tathmini ya athari ya mazingira. Sheria inakataza mtu yeyote kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka chanzo cha maji,” alisema Mushi.
Alisema Mbowe alipewa miezi minne kuondoka kwa hiyari yake lakini alidharau mamlaka halali ya Serikali na pia kizuizi cha Nemc alichopewa Juni 7, kikimtaka kusitisha shughuli hizo.
“Hiyo barua yetu ya kizuizi iliambana na penalti (adhabu) ya Sh18 milioni kwa kukiuka hayo maagizo aliyopewa. Tumetekeleza hili zoezi la kuharibu miundombinu lakini ataligharamia,” alisema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nshara, Emanuel Mbowe alisema shamba hilo lilikuwa linatoa ajira kwa wananchi wanaolizunguka na kwamba kufungwa kwake ni pigo.
0 comments:
Post a Comment