Wednesday, 14 June 2017

ACACIA waelezea usajili wao

KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Acacia, imesema kuwa inafanya kazi nchini kwa misingi ya sheria na Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CMSA) inatambua uwepo wake.

Kauli hiyo imekuja baada ya juzi taarifa ya pili ya wachumi na wanasheria iliyofanya uchunguzi wa mchanga wa madini katika makontena yalizuiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi, kubainisha kuwa kampuni hiyo haina kibali na inafanya kazi kinyume na sheria.


Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo jana pia imesema kuwa Acacia itafanya mkutano na wanahisa wake kesho kutoa ufafanuzi zaidi juu ya sakata zima.

Kampuni hiyo ilieleza kuwa migodi yake ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara inaendeshwa kisheria.

“Acacia inapenda kuthibitisha kwamba inaendelea kufanya kazi katika migodi yake mitatu ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara.

“Migodi hii yote inamilikiwa na kuendeshwa na makampuni ambayo yamesajiliwa Tanzania kisheria; Bulyanhulu Gold Mine Limited, Pangea Minerals Limited na North Mara Gold Mine Limited ambayo yana leseni maalumu kwa kila mgodi,” inasomeka sehemu ya taarifa katika tovuti ya Acacia ambayo gazeti hili iliiona jana.

Taarifa hiyo iliendelea kueleza: “Kampuni hizi zinamilikiwa na Acacia ambayo imesajiliwa nchini Uingereza ingawa umiliki huu si wa moja kwa moja (indirectly owned).

“Muundo huu ni wa uwazi, upo kisheria na huwekwa wazi katika taarifa zetu za hesabu za mwaka ambazo hukaguliwa kwa mujibu wa taratibu za kimataifa.”

Taarifa hiyo iliendelea kufafanua kwamba utaratibu huo wa umiliki uliwekwa wazi kwa CMA wakati Acacia ikijioredhesha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2011.

“Muundo huu ni sehemu ya taarifa ambayo ilipitishwa na CMSA kwa ajili ya kujiorodhesha DSE. Tangu kujisajili DSE kilichobadilishwa ni jina la Acacia kutoka African Barrick Gold Plc kuwa Acacia Mining Plc,” inasema taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Acacia wametangaza kufanya mkutano na wanahisa wake kwa mtandao kesho kutoa ufafanuzi zaidi juu ya sakata zima.

Walipofuatwa DSE kutoa maelezo ni kwa vipi kampuni ambayo haina usajili kuweza kujiorodhesha na kuuza hisa, walisema wao si wasemaji kwa kuwa mchakato wa kujiorodhesha huongozwa na kusimamiwa na CMSA na hivyo kumshauri mwandishi awasiliane nao.

Mwandishi alipowasiliana na  Ofisa Habari wa CMSA, Charles Shirima, alisema mtu aliyekuwa akishughulikia suala hilo alikuwa safarini Dodoma na kumtaka mwandishi awasiliane naye leo.

0 comments:

Post a Comment