Thursday, 8 June 2017

Chelsea: Diego Costa amesema klabu hiyo inataka kumuuza

Diego CostaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionCosta amesema angependa sana kurejea Atletico Madrid
Mshambuliaji wa klabu ya Chelsea Diego Costa amesema amefahamishwa na meneja wa klabu hiyo Antonio Conte kwamba hayupo tena katika mipango ya klabu hiyo.
Costa, 28, alifunga mabao 20 katika emchi 35 alizocheza Ligi ya Premia na kusaidia Blues kushinda taji la ligi hiyo lakini sasa anaonekana kukaribia kuondoka Stamford Bridge.
"Mimi ni mchezaji wa Chelsea, lakini hawanitaki huko," Costa amesema.
"Antonio Conte amenijulisha kupitia ujumbe kwamba siendelei Chelsea na mambo yako hivyo. Conte alisema kwamba hanitegemeu msimu ujao."
Akiongea baada ya sare ya 2-2 kati ya Uhispania na Colombia Jumatano, Costa aliongeza: "Uhusiano wangu na mkufunzi huyo umekuwa mbaya msimu huu. Ni aibu, tayari nimesambaza ujumbe huo kwa watu wa Chelsea waamue.
"Lazima utafute timu (ya kuchezea)."
Costa ambaye ni mzaliwa wa Brazil lakini huchezea timu ya taifa ya Uhispania alijiunga na Chelsea kutoka Atletico Madrid kwa £32m mwaka 2014.
Alikaa misimu minne Atletico na alikuwa amedokeza kwamba huenda akarejea katika klabu hiyo.
Lakini klabu hiyo ya La Liga imepigwa marufuku kununua wachezaji hadi Januari.
"Kukaa miezi mitano bila kucheza? Sijui, ni kizungumkuti, lakini watu wanajua kwamba naipenda sana Atletico na kwamba huwa napenda kukaa Madrid," Costa amesema.
"Litakuwa jambo zuri kwangu kurejea, lakini ni vigumu kukaa miezi minne au mitano bila kucheza. Ni mwaka wa Kombe la Dunia na kuna mengi ya kufikiria. Nahitaji tu kucheza, hivyo tu."
Diego CostaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionCosta alifunga mabao 22 katika mechi 42 mashindano yote msimu uliomalizika majuzi
Januari, Costa aliachwa nje ya kikosi cha Chelsea kilichosafiri kucheza mechi ugenini Leicester baada yake kukorofishana na mkufunzi wa mazoezi.
Hilo lilitokea baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba alikuwa amepata ofa kutoka China ya kulipwa mshahara wa £30m kwa mwaka. Wakati huo, Chelsea walisema hawakuwa na nia ya kumuuza.
Baadaye Januari, mmiliki wa Tianjin Quanjian alisema juhudi zao za kutaka kumnunua Costa zilitatizwa na sheria mpya kuhusu wachezaji wa kutoka nje Ligi Kuu ya Uchina.
Kuanzia msimu ujao, klabu za Uchina zinaruhusiwa kuchezesha wachezaji watatu pekee kutoka nje ya nchi kwenye mechi badala ya wanne kama ilivyokuwa awali.
 source:bbc

0 comments:

Post a Comment