Bocco (kulia) akikabidhiwa jezi ya Simba na rais wa klabu hiyo Evans Aveva, imeteka vichwa vya habari vya mitandao mbalimbali ambapo mashabiki wa Simba wameonyesha kufurahishwa na usajili huyo.
UONGOZI wa Simba, jana umetangaza rasmi kumsajili aliyekuwa mshambuliaji wa Azam, John Bocco baada ya tetesi za muda mrefu kuhusiana na suala hilo. Mara baada ya zoezi hilo, Bocco amefunguka kuwa atahakikisha anaendeleza moto wake wa kuzifumania nyavu kwa timu yoyote ile atakayokutana nayo kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara ikiwemo Yanga.
Bocco amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Azam sambamba na aliyekuwa kipa wa timu hiyo, Aishi Manula na beki wa kulia, Shomari Kapombe ambao wote wamejiunga kwa mikataba ya miaka miwili.
Akizungumza na Championi Jumatano, Bocco alisema kuwa tangu ajiunge na Simba baada ya miaka 11 ndani ya Azam, kamwe hawezi kuwa adui kwa mashabiki wa timu hiyo kutokana na kuwafunga mara nyingi.
“Unajua kazi yangu kubwa ni kufunga, sasa sidhani kama ukiifunga timu fulani halafu ukajiunga nayo wanakuwa maadui zako. Ile ilikuwa natimiza majukumu ya kazi yangu wakati nipo Azam kama nilivyokuwa nazifunga timu zingine, hata sasa hivi nipo Simba nikikutana na timu yoyote nitaifunga tu kama Mungu akipenda.
“Nashukuru Mungu, uongozi na mashabiki wa Simba kwa jumla, kikubwa nimekuja kufanya kazi kwa sababu naamini watasajili wachezaji wengine wazuri, nguvu niliyokuwa nayo ambayo nitaiongeza kwa wenzangu tutaweza kufanya vizuri, naomba Mungu anisaidie maisha ya mafanikio zaidi kuliko nilipotoka,” alisema Bocco. Bocco anaungana na Aishi Manula, Shomary Kapombe, Yusuph Mlipili na Jamal Mwambeleko kuwa wachezaji wapya waliosajiliwa na klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao ambapo ukiondoa mashindano ya ndani, Simba itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
0 comments:
Post a Comment