Tuesday, 13 June 2017

Mwanamke ajichinja kwa chupa

MWANAMKE aliyefahamika kwa jina la Saada Elias (24) mkazi wa Mtaa wa Mabambase katika Manispaa ya Shinyanga alifariki dunia kwa kujikata koromeo kwa chupa ya soda.

Mwanamke huyo alijiua kwa chupa ikiwa ni muda mfupi baada ya kunyang’anywa kisu wakati akijaribu kujichinja, kwa madai ya kuandamwa na ugumu wa maisha.

Tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita majira ya saa tisa usiku, wakati mwanamke huyo akiwa chumbani kwake na mdogo wake wa miaka 12 na mtoto wake wa miaka minne.

Imeelezwa kuwa alichukua uamuzi wa kujichinja kwa kisu shingoni, lakini mdogo wake huyo alishtuka kutoka usingizini na kumpokonya silaha hiyo; ndipo akachukua chupa ya soda na kujikata koromeo papo hapo.

Akisumulia tukio hilo, Peter Maduhu ambaye ni mpangaji mwenzake alisema baada ya mdogo wa mwanamke kupiga kelele ya kuomba msaada kuwa dada yake amejichinja, ndipo walipoamka kutoa msaada, lakini walipoingia ndani walimkuta tayari ameshajikataa koromeo kwa kutumia chupa ya soda.

Alisema kabla ya tukio hilo marehemu alikuwa akilalamika kuwa anaumwa kwa muda mrefu ugonjwa ambao hakuwa akiutaja.

Aidha, alisema Maduhu, marehemu alikuwa akidai kuwa hakuna ndugu wala mtu wa kumsaidia licha ya kuandamwa na ugumu wa maisha.

“Marehemu alikuwa kifanya shughuli ya mamalishe," alisema Maduhu "lakini siku ambayo alikuwa akitaka kujiua mdogo wake alikuwa akisema dada yao yupo kazini."

"Kumbe amejifungia ndani na ilipofika majira hayo ya saa tisa usiku, ndipo tukasikia kelele za mtu akiomba msaada na tulipofika chumbani kwake alikuwa tayari amejikata koromeo.”

Baba mzazi wa marehemu, Elias Ruleja ambaye ni mkazi wa mkoani Kagera alisema mtoto wake huyo alitoweka nyumbani mwaka jana kuja kuishi Shinyanga bila ya yeye kufahamu hadi alipopokea taarifa ya kifo chake kutoka kwa majirani zake.

Alisema amehuzunishwa sana na kifo hicho, huyo akiwa mtoto peke aliyekuwa amebaki kutokana na kaka yake kufariki miaka mingi iliyopita.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Jumanne Muliro alithibitisha juzi kutokea kwa tukio hilo, na akaeleza kwamba hakuna mtu yeyote ambaye anashikiliwa kuhusiana nacho.

source:muungwana

0 comments:

Post a Comment