Sunday, 21 May 2017

FEDHA ZA RAMBIRAMBI ZATUMIKA KUJENGA HOSPITALI


JINAMIZI la matumizi ya fedha za rambirambi kwenda kwa familia za wanafunzi limegeuka kaa la moto kwa kuamuliwa sehemu ya fedha hizo zipelekwe kukarabati Hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru.

Fedha hizo ni zinazotakiwa kuwasilishwa  kwa familia za   wanafunzi 33,   walimu na dereva wa basi la Shule ya Lucky Vincent, waliofariki katika ajali iliyotokea wiki chache zilizopita.
Habari zinasema, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo anadaiwa kuwaita wazazi wafiwa akiwataka wakubali Sh milioni 56 walizotakiwa kupewa, zielekezwe kufanya mambo mengine tofauti.
Gumba anadaiwa kutaka fedha hizo zielekezwe katika mambo matatu ambayo ni  kuboresha wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), kujenga kitengo cha magonjwa ya akili au kuboresha chumba cha kuhifadhia maiti katika  Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Akizungumza mjini hapa jana baada ya Ibada maalumu ya kuombea majeruhi walioko  Marekani na wazazi waliopoteza watoto wao kwenye ajali hiyo, mmoja wa wazazi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema   wameamua kujitoa kwenye kamati ya kupanga matumizi ya Sh milioni 56 zilizobaki ili kuipa serikali fursa ya kupanga yenyewe matumizi ya fedha hizo.
 
Mzazi huyo aliyeomba kutotajwa gazetini kwa sababu za usalama wake,  alisema wameamua kujitoa kwenye kamati hiyo baada ya kutoona sababu na umuhimu wa kuwapo kwao.
“Mambo mengi sana yalishafanywa na kukamilika, sisi tuliitwa Mei 16, mwaka huu kwa mkuu wa mkoa na kusomewa taarifa ya fedha zilizotumika.
“Baada ya kikao hicho ikaundwa kamati ya kusimamia Sh milioni 56 zilizokuwa zitumike kwa ajili ya kumbukumbu ya watu 35 waliokufa.
"Nilichaguliwa kuwa mmoja wa wanakamati tukiwa wanaume wawili na wanawake Wawili, tuungane na kamati iliyopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa….wenzangu walikwenda kwenye kikao mimi sikwenda sikuwa na taarifa.
“Sh milioni 56 zilizobakia tuliambiwa tuangalie zifanye nini  huku tayari  mapendekezo yakiwa ni Hospitali ya Mount Meru kwamba zifanye maboresho chumba cha kuhifadhi maiti, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) au kuweka kitengo cha magonjwa ya akili badala ya wagonjwa kupelekwa Hospitali ya Mawenzi au Mirembe Dodoma,” alisema mzazi huyo.
Mzazi huyo alidai kwamba Ijumaa   iliyopita walikwenda Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa na kueleza nia yao ya kutoendelea kwenye kamati hiyo kama sehemu ya wazazi waliofiwa.
“Tumeona ni vema serikali iendelee na utaratibu wote kwa sababu kitendo pia cha wazazi wafiwa kuwekwa chini ya ulinzi na  polisi kule shuleni Lucky Vincent kilitusukuma kuona hatuna sababu ya kuwa sehemu ya kamati,” alisema mzazi huyo na kuongeza:
“Tuliitwa baada ya mambo yote kukamilika, kwa ujumla hatukuridhishwa na fedha za rambirambi kubadilishiwa matumizi.
“Kubwa linalotusikitisha ni kuambiwa kwamba fedha hizo za rambirambi zimetokana na nguvu ya uchangishaji ya mkuu wa mkoa kwa hiyo wana haki ya kuzifanyia utaratibu wao wenyewe,” alisema.
Taarifa   inayodaiwa kutolewa na Gambo iliyosambaa katika mitandao mbalimbali ya  jamii jana, ilimnukuu mkuu huyo wa mkoa akisema   ameona ni vema nguvu kubwa ikapelekwa kuwahudumia majeruhi watatu wanaopatiwa matibabu  Marekani.
Kupitia taarifa hiyo,  Gambo alisema hadi Mei 20 mwaka huu kutokana na wadau kuendelea kuchangia rambirambi, zimepatikana zaidi ya Sh milioni 67.9, hivyo fedha hizo zitatumika kuwahudumia majeruhi hao.
“Kutokana na wadau kuendelea kuchangia tumebakiwa na Sh milioni 67,993,885, kwa mantiki hiyo busara imeelekeza kuwa nguvu kubwa sasa ipelekwe kwenye kuwahudumia majeruhi maana hata tufanyeje wale ambao Mungu kwa mapenzi yake amewachukua hatuna namna tena ya kuwarudisha,” alisema na kuongeza.
"Jumatatu Mei 22 mwaka huu tutazitumia familia za majeruhi na madaktari wetu waliojitoa kuwasindikiza majeruhi   Dola za Marekani 20,000 (Sh 44,720,000),    kila familia itapata Dola 5,000, daktari Dola 2500 na muuguzi Dola 2500, kama sehemu ya kuendelea kuwafariji na kuwapunguzia changamoto huko ugenini".
Gambo alisema baada ya matumizi hayo zitabaki zaidi ya Sh milioni  22.2 huku hali za majeruhi zikiendelewa kuangaliwa na  fedha zilizobaki zitaendelea kuwekewa utaratibu kupitia timu ya wafiwa wane walioteuliwa na wafiwa wenzao kushirikiana na serikali kuhakikisha mapato na matumizi ya suala hilo yanaeleweka kwa umma.
Alisema pia kuwa  ofisi yake imehitimisha rasmi hatua ya kupokea rambirambi ili ipate muda zaidi wa kufuatilia mustakabali wa majeruhi   walioko Marekani kwa
matibabu.
Akijibu hoja za fedha kuchepushwa na kupelekwa katika ujenzi wa hospitali, Gambo aliwashangaa watu wanaojadili hewa kwani hakuna fedha iliyopelekwa katika ujenzi.

“Mnajadili hewa badala ya taarifa sahihi. Hakuna hela iliyokwenda Mount Meru Hospitali. Mtu ukiwa mnafiki ukiwa kijana ukizeeka unakuwa mchawi,” alijibu Gambo katika moja la magropu ya mtandao wa kijamii wa WhatApp

MEYA

Katika ibada ya jana, mbali na wazazi na walezi waliopoteza watoto wao  katika ajali hiyo, wengine weliokuwapo ni Meya. Calist Lazaro    madiwani wa Halmashauri ya Jiji hilo na wengine kutoka Halmashauri ya Meru.
Akizungumzia hatua ya kamati hiyo kujitoa kabla ya kufanya shughuli iliyokusudiwa, Lazaro alisema kwa vile  suala hilo lina ukakasi, wananchi wa Arusha na viongozi wengine ambao hawakushirikishwa katika mchakato huo, hawatashiriki jambo lolote kuhusu fedha za rambirambi zilizobaki kwa Gambo.
"Nashukuru Mungu amesaidia leo tumehitimisha ibada maalum ya kuwaombea watoto wetu wanaotibiwa Marekani ila kwa uamuzi huo wa wazazi wetu ambao  wamechukizwa na vitendo ambavyo Mkuu wa Mkoa anaendelea kuvifanya, wa kuamua kujitoa kwenye kamati, tunawaunga mkono na hatutaingilia jambo hili ambalo lilikwisha kuharibiwa,” alisema.

source: mtanzania

0 comments:

Post a Comment