Baraza la Madiwani wamemuweka kiti moto Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba, baada ya kujenga chini ya kiwango mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya takataka katika dampo la Buhongwa.
Madiwani wa jiji hilo wanamtuhumu Kibamba kujenga chini ya kiwango majengo matatu ya mradi huo ikilinganishwa na thamani halisi ya fedha iliyotolewa katika mradi huo uliopo kata ya Buhongwa.
Mradi huo wa uboreshaji miundombinu pia unatekelezwa katika majiji matano ya Mbeya, Dar es Salaam, Tanga, Arusha na Mwanza na baadhi ya miji, unaofadhiliwa na Benki kuu ya Dunia (WB), tayari mradi huo umetumia zaidi ya Sh. 400 milioni.
Hata hivyo, ili Benki ya Dunia iweze kufadhili mradi husika lazima halmashauri husika iwe imetenga eneo ambalo limelipiwa fidia na limeandaliwa vizuri na kujengwa jengo la kuhudumia gari na mitambo, jengo la ofisi na mzani na jengo la kufanya usafi wa mitambo.
Ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa dampo hilo la kisasa bado unasuasua kutokana na kati ya wananchi 70 waliokuwa na viwanja eneo hilo waliolipwa ni 40 (Sh. 360 milioni) huku wengine 30 bado wanaendelea kuidai halmashauri ya jiji Sh. 270 milioni.
Madiwani hao chini ya Meya wa Jiji hilo, James Bwire walishtukia mchezo huo baada ya kuchunguza na kubaini mradi huo unatekelezwa chini ya kiwango kutokana na kampuni hizo mbili ni mkurugenzi ni mmoja wa wamiliki.
Kampuni zilizopewa zabuni bila kupitia taratibu za utoaji wa zabuni ni Majee Investment LTD na Tinde Contractors LTD (za shinyanga) ambazo zinajenga majengo matatu ya kuhudumia magari, Jengo la ofisi na mzani na jengo la kuoshea magari (Car wash).
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Kibamba, Aprili 5, mwaka huu baada ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, kufanya ziara katika dampo hilo, amesema kwamba, majengo matatu yamegharimu kiasi cha Sh. 435 milioni huku bado zoezi la ujenzi likiendelea.
Katika taarifa hiyo kwa mkuu huyo wa mkoa iliainisha kwamba jengo kuhudumia magari (Car Services) limegharimu Sh. 131 milioni, jengo la ofisi na mzani 165 milioni na jengo la kuishea magari car wash 139 milioni.
Mmoja wa madiwani (jina linahifadhiwa) ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya fedha na uongozi, aliuambia mtandao huu kuwa, baada ya kufanya ziara katika mradi huo Aprili 23, mwaka huu walibaini thamani ya fedha iliotolewa na mkurugenzi haiendani na uhalisia wa gaharama zilizotumika kila jengo.
Amesema kuwa anashangazwa kuona mkurugenzi huyo, akizipatia zabuni kampuni mbili zinazomilikiwa na mtu mmoja kujenga mradi huo kinyume na taratibu na tayari zimelipwa kiasi cha Sh. 199 milioni na bado jiji linadaiwa Sh. 219 milioni.
“Hizi kampuni inasemekana mkurugenzi (Kiomoni Kibamba) ni mmoja wa wamiliki wake na kampuni hizi zilikuwa Shinyanga ambako zimejenga miradi chini ya kiwango lakini tunashangaa zimepewa zabuni,” amesema Diwani huyo.
Diwani huyo amedai kwamba katika ziara yao iliyoongozwa na Meya wa Jiji, wajumbe wa kamati hiyo, walishtushwa na taarifa ya Kibamba na kuomba meya kuiwasilisha hoja katika kikao cha baraza la madiwani.
Hata hivyo amedai kwamba katika kikao cha baraza la madiwani kiliazimia mkuu wa mkoa wa Mwanza aunde tume ya kuchunguza gharama halisi iliyotumika kutekeleza mradi huo ikizingatiwa fedha ya awali ya mradi huo ni ya wananchi.
Pia aliendelea kueleza kwamba, kamati ilibaini kampuni hizo mbili za ukandarasi hazina vifaa na badala yake zilikuwa zinatumia magari na mitambo ya jiji kwa ajili ya kusafisha eneo la dampo kwa agizo la Mkurugenzi Kiomoni Kibamba.
“Jiji na watendaji wake wanafahamu kwamba mkandarasi anatakiwa kutekeleza kazi hiyo kwa vifaa vyake kwenye eneo la mradi lakini wao wanatumia vya halmashauri na kusababisha hasara ya mafuta na mitambo kinyume na taratibu za zabuni,” amesema diwani huyo.
Hata hivyo diwani huyo amesema kuwa wanachokisubiri hivi sasa ni taarifa za tume ilioundwa na mkuu wa mkoa kuchunguza tuhuma hizo na thamani halisi ya ujenzi wa majengo hayo.
Aprili 5, mwaka huu, Mkurugenzi Kibamba, alikiri mbele ya mkuu wa mkoa huo na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Marry Tesha, kwamba alizileta kampuni hizo kutoka mkoani Shinyanga, kutekeleza mradi huo.
Hivi karibuni katika ziara ya mkuu wa wilaya ya Nyamagana, mkurugenzi huyo alidai kwamba mradi huo tayari umetumia Sh. 500 milioni na kwamba wanatarajia kupokea kiasi cha Sh. 18 bilioni kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kujenga madampo ya kisasa na barabara za katikati ya jiji.
Tayari inaelezwa kwamba kampuni hizo, zilishawahi kufanya kazi iliotolewa na halmashauri ya Shinyanga vijijini na kupata hasara baada ya kutekeleza mradi uchimbaji mabwawa na miradi mingine iliotolewa na halmashauri hiyo ilitekelezwa chini ya kiwango.
0 comments:
Post a Comment