Wabunge waandamizi nchini Marekani wamemtaka rais Donald Trump kusalimisha mazungumzo yoyote yaliorekodiwa kati yake na aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la FBI James Comey aliyemfuta kazi.
Kiongozi wa Democrats katika bunge la seneti Charles Schumer alionya kuwa uharibifu wa kanda hizo utakuwa uvunjaji wa sheria.
Naye Seneta wa Republican Lindset Graham alisema kuwa Ikulu ya Whitehouse inahitaji kuwa wazi kuhusu iwapo kulikuwa na kanda zozote za rekodi za mazungumzo hayo au la.
Matamshi hayo yanajiri baada ya bwana Trump kusema katika mtandao wake wa Twitter matamshi yanayoonekana kuwa vitisho kwa mkuu huyo wa zamani wa FBI.
Alimuonya Comey wiki iliopita dhidi ya kuzungumza na vyombo vya habari akisema natumai hakuna rekodi za mazungumzo yetu.
Ikulu ya Whitehouse haijathibitisha wala kukana kuwepo kwa kanda hizo.
Bwana Schumer pia alionya kwamba masenata wa chama cha Democrats watakataa kumuunga mkurugenzi mpya wa FBI hadi pale mtaalam atakapochaguliwa kuchunguza hatua ya Urusi kuingilia maswala ya Marekani katika uchaguzi uliopita.
FBI inachunguza madai hayo pamoja na ushirikiano wa Urusi na kampeni ya rais Trump.
Rais Trump amekana uhusiano wowote na anasema bwana Comey amemhakikishia kwamba hachunguzwi.
Anasema kuwa alimpiga kalamu bwana Comey kwa sababu alikuwa ameshindwa kufanya kazi vizuri.
Wanachama wa Democrats wameshutumu Trump kwa kumfuta kazi Comey ili kujaribu kusitisha uchunguzi wa FBI.
source:bbc
0 comments:
Post a Comment