YANGA juzi ilipiga hodi kwa wadhamni wao Kampuni ya SportPesa kuomba watanguliziwe Sh milioni 400 kwa ajili ya mishahara ya wachezaji wake. Timu hiyo, inadaiwa mishahara ya miezi mitatu na wachezaji wake walioiwezesha kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo ikiwemo msimu uliopita.
SportPesa hivi karibuni iliingia mkataba waudhamini wa miaka mitano na Yanga ambapo kila mwaka itakuwa ikipata Sh milioni 995.
Bosi mmoja wa Yanga aliliambia Championi Jumamosi kuwa, wameifuata SportPesa ili wawape fedha hizo kwa ajili ya kuwalipa mishahara wachezaji ili waanze haraka kambi ya mazoezi kujiandaa na michuano ya SportPesa Super Cup.
Alisema nusu ya wachezaji wamegomea kambi ya timu hiyo ila wameahidi kujiunga nayo endapo watalipwa malimbikizo yao ya mishahara ya miezi mitatu, miongoni mwao ni straika Amissi Tambwe.
“Kama mmoja wa viongozi wa Yanga, nilitoa mapendekezo kwa wenzangu na kamati yetu ya utendaji kwenda kuwaomba SportPesa watutangulizie shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuwapa wachezaji wetu madai ya mishahara yao ya miezi mitatu.
“Mambo yanaenda vizuri na hivi karibuni tunatarajia kumaliza kila kitu.
“Ilikuwa lazima twende SportPesa kuomba fedha hizo, kama unavyojua wao ndiyo waandaaji wa michuano hiyo mipya tutakayoshiriki, hivyo tumekutana na kuahidi kulifanyia kazi hilo na mara litakapomalizika basi tutaanza kambi haraka,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa kuzungumzia ishu hiyo, alisema: “Wachezaji wanaidai timu mishahara ya miezi mitatu, na viongozi tunatafuta fedha na muda wowote tutawalipa.”
0 comments:
Post a Comment