Friday, 2 June 2017

Kesi ya Lissu yakwama kuendelea Kisutu

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu   

Dar es Salaam.  Kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu  imeshindwa kuendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  kwa sababu wakili wa Serikali anayeindesha, Mohammed Salum amepangiwa kazi nyingine.

Kwa mujibu wa kesi hiyo ambayo ipo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka  leo ilipaswa kuendelea kusikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfey Mwambapa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa ameiambia mahakama leo Ijumaa kuwa kesi ilipangwa kusikilizwa lakini wakili Salum anayeiendesha amepangiwa kazi nyingine  hivyo akaomba iahirishwe.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, kesi imeahirishwa hadi Juni 16, 2017.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwanasheria wa Chadema anadaiwa kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Anadaiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa kauli za uchochezi kuwa:

“Mamlaka ya Serikali mbovu ni ya kidiktekta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote, huyu dikitekta uchwara lazima apingwe kila sehemu. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani ya giza nene.’’

Katika kesi hiyo, tayari mashahidi wawili  wa upande wa mashtaka Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Kimweli na Staff Sajenti Ndege wamekwishatoa ushahidi wao.

0 comments:

Post a Comment