Aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema Serikali ilikuwa na mpango wa kujenga mtambo wa kuchenjua madini tangu muda mrefu.
Amesema hayo leo Ijumaa bungeni wakati akifafanua tuhuma zinazotolewa kwa viongozi wa wizara hiyo waliokuwapo wakati mikataba ya madini inasainiwa kwamba hawakufanya chochote kuepusha wizi na udanganyifu unaoendelea kwenye sekta ya madini.
"Kabla sijajiuzulu miaka mitano iliyopita tulikuwa na mpango wa kujenga smelter nchini. Ingawa tuliambiwa gharama ni kubwa ila tulikuwa tunatafuta namna nzuri ya kufanikisha hilo. Hii ndiyo namna ya kufanikisha udhibiti wa sekta hii. Tulikuwa na nia," amesema.
Kauli ya Ngeleja aliyekuwa waziri wa wizara hiyo katika Serikali ya Awamu ya Nne imekuja wakati kukiwa na malalamiko kuwa viongozi waliopita kwenye wizara hiyo hawakuchukua hatua kuhakikisha suala la mchanga wa madini kusafirishwa nje linafanyiwa kazi.
Tangu Rais John Magufuli azuie usafirishwaji wa mchanga wa madini kwenda nje na kuagiza ukaguzi wa makontena 277 yaliyoko bandarini kumekuwa na maoni tofauti kuhusu uamuzi huo lakini ripoti ya kamati ya ukaguzi ilipotolewa ikaleta maneno zaidi.
Wabunge kama Tundu Lissu(Singida Mashariki) walitaka baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo, mawaziri wengine wote waliopita wizara hiyo tangu mwaka 1998 wachukuliwe hatua.
0 comments:
Post a Comment