Polisi nchini Musumbiji wameonya kuwa wamaume wenye vipara huenda wakalengwa kwenye mashambulizi yanayohusiana na uchawi, pamoja na matambiko fulani, baada ya kuuliwa kwa wanaume wawili kama hao mwezi uliopita.
Wanaume hao wawili wenye upara na ambapo mmoja wao alipatikana akiwa amekatwa kichwa na viungo vya mwili vikiwa vimetolewa, waliuliwa katika mkoa wa Zambezi.
"Mwezi uliopita mauaji ya watu wawili wenye vipara yalisababisha kukamatwa kwa washukiwa wawili," msemaji wa polisi Inacio Dina, alisema kwenye mkutano wa waandishi wa habari mjini Maputo.
Mwandishi wa BBC mjini Maputo anasema kuwa baadhi ya watu wana imani potovu kuwa watu wenye vipara wako na dhahabu kwenye vichwa vyao.
Visa vya kuuliwa watu wenye upara kwa maswala ya uchawi havijaripotiwa siku za nyuma.
Washukiwa ni vijana wa Msumbiji, waliowaambia polisi kuwa viungo hivyo vingetumiwa kwa uchawi na matambiko nchini Tanzania na Malawi.
Tanzania inafahamika duniani kwa watu wenye matatizo ya ngozi kuuwawa na viungo vyao kutumika kwenye matambiko ya kichawi.
Hapo awali nchini Tanzania ilishawahi kutokea watu wenye vipara kutafutwa na kuuawa kwa imani za kishirikina.
source:bbc
0 comments:
Post a Comment