Sunday, 21 May 2017

Trump kuzuru Israel chini ya ulinzi mkali

Benjamin Netanyahu na Donald Trump (15/02/17)
Rais wa Marekani Donald Trump anazuru Israel na Maeneo ya Wapalestina leo, akiendelea na ziara yake ya kikazi katika maeneo ya Mashariki ya Kati.
Atafika maeneo hayo akitokea Saudi Arabia, mshirika muhimu wa Marekani, ambako alitoa hotuba katika mkutano mkuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu.
Bw Trump anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Israel na Palestina katika kipindi cha siku mbili atakazokuwa eneo hilo.
Rais huyo amesema kupatikana kwa mkataba wa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina yatakuwa mafanikio makubwa, lakini hakusema mkataba kama huo unafaa kuchukua mwelekeo gani.
Amesema angependa sana pande zote mbili ziamue kuhusu mkataba huo wa amana kwa mashauriano ya moja kwa moja.
Katika mkutano mkuu wa viongozi wa Kiislamu na Kiarabu mjini Rihadh siku ya Jumapili, Bw Trump aliwataka viongozi hao kuwa kwenye mstari wa mbele katika kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu na wapiganaji wenye itikadi kali na "kuwafurusha kutoka kwenye dunia hii."
Aliitaja moja kwa moja Iran na kusema kwamba imekuwa "ikichochea mizozo ya kidini na ugaidi" katika kanda hiyo kwa miongo mingi.
Bw Trump pia alikariri tena kwamba anaamini amani kati ya Waisraeli na Wapalestina inaweza kupatikana.
Rais huyo wa Marekani amekuwa akichukuliwa sana kuwa muungaji mkono mkubwa wa Israel kuliko mtangulizi wake Barack Obama.
Amechukua msimamo usio mkali kuhusu suala tata la Israel kujenga makazi ya walowezi maeneo ya Wapalestina na kudokeza kwamba upanuzi wa makao hayo na si kuwepo kwa makao yenyewe, unaweza kuwa ndio kikwazo katika kutafuta amani.
Zaidi ya Wayahudi 600,000 huishi katika makao makazi 140 ya walowezi ambayo yamejengwa tangu Israel ilipotwaa maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Jerusalem mwaka 1967, maeneo ambayo Wapalestina huyachukuliwa kuwa sehemu ya "taifa litakaloundwa" la Wapalestina.
Makazi hayo ni haramu chini ya sheria za kimataifa, lakini Israel hupinga hilo.
Rais huyo pia ametoa ishara za kukanganya kuhusu mji wa Jerusalem, na kuahidi kuhamishia ubalozi wa Israel mjini humo kutoka Tel Aviv, hatua iliyowakera Wapalestina lakini ikawafurahisha sana Waisraeli.
Hata hivyo, baadaye alionekana kulegeza msimamo huo, na Waziri wa Mambo ya Nje Rex Tillerson majuzi aliambia NBC News kwamba Bw Trump bado analitafakari jambo hilo.

Mzozo kuhusu Jerusalem

Israel huuchukulia mji wote wa Jerusalem kuwa mji wake mkuu, nao Wapalestina huchukulia maeneo ya mashariki ya mji huo kuwa makao makuu yake.
Jamii ya kimataifa haijatambua umiliki wa Israel wa mji wa Jerusalem na mataifa mengi yana afisi za kibalozi mjini Tel Aviv.
Kumekuwa na wasiwasi kidogo Israel kabla ya ziara ya Bw Trump kutokana na baadhi ya matamshi ya maafisa wake.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amepuuzilia mbali maneno ya Bw Tillerson kwamba kuhamishwa kwa ubalozi wa Marekani kunaweza kuathiri shughuli ya kutafuta amani eneo hilo. Afisa wa kibalozi wa Marekani naye aliwakera Waisraeli aliposema kuwa Ukuta wa Magharibi, moja ya maeneo matakatifu zaidi katika dini ya Kiyahudi haumo "katika maeneo yenu (Waisraeli) bali ni sehemu ya Ukingo wa Magharibi".
White House baadaye ilisema tamko la afisa huyo wa kibalozi "hayawakilishi msimamo wa Marekani".
Ziara ya Bw Trump inajiri siku chache baada ya taarifa kusema Bw Trump alifichua taarifa za siri kwa Warusi ambazo huenda zilitoka kwa mdokezi kutoka Israel.
Kisa hicho kimeibua maswali kuhusu usiri na usalama wa habari za kijasusi zinazokabidhiwa Marekani na Israel.
Operesheni kubwa ya kiusalama inaendelea kabla ya ziara ya Bw Trump, ambaye anatarajiwa kukutana na Bw Netanyahu mjini Jerusalem Jumatatu na baadaye akutane na kiongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Bethlehem Jumanne

Ajenda ya ziara ya Trump

Bw Trump pia atazuru Brussels, Vatican, naSicily.

Ziara hiyo imegubikwa na mtafaruku wa kisiasa nchini mwake, sana kutokana na hatua yake ya kumfuta kazi mkuu wa FBI James Comey.
source:bbc

Related Posts:

  • Nyumba zateketea kwa moto Sengerema Sengerema. Nyumba za wavuvi ambazo idadi yake haijajulikana hadi sasa katika kisiwa cha uvuvi cha Nyamango Kata ya Bulyaheke  halmashauri ya Buchosa wilayani hapa, zinateketea kwa moto ambapo chanzo chake hakijajul… Read More
  • Polisi watangaza dau la Mil. 60 Ukiwakamatisha hawa JESHI la Polisi mkoa wa Pwani limetangaza zawadi ya Sh. milioni tano kwa mwananchi ambaye atafanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 12 ambao limedai wanajihusisha na mtandao wa mauaji yanayoendelea katika Wilaya za Kibiti, Mku… Read More
  • Mtaji wa Soko la Hisa DSM waporomoka Ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) umepungua kwa Shilingi Bilioni 380 kutoka Shilingi Trilioni 20.2 wiki iliyopita hadi Shilingi Trilioni 19.9 kwa wiki iliyoishia Mei 19 mw… Read More
  • Mbunge atinga bungeni na rundo la risiti Dodoma.Mbunge wa Viti maalum (Chadema), Rhoda Kunchela aliwasilisha bungeni furushi la risiti za mwenge wanazodaiwa kuchangishwa kwa nguvu, walimu na wafanyabiashara.Mbunge Kunchela aliomba kutoa hoja ili ijadiliwa na Bunge … Read More
  • Nape amemjibu Makonda, Picha limeanza upyaaa Siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kuhojiwa na kituo cha Star Tv kuhusu mambo kadha wa kadha likiwemo suala la uvamizi wa Clouds Media na kusema Hakupaswa kumuingilia kwakuwa wote ni watumishi... Basi Nape ame… Read More

0 comments:

Post a Comment